Mastaa Azam wawekewa milioni 300 waigomee Simba 

Muktasari:

  • Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 25 ikishinda 17, imetoka sare mechi sita na kupoteza michezo miwili wamekusanya pointi 57 ikiiacha nyuma kwa pointi nne Simba ambayo inashindania nafasi hiyo kulingana na kuachana kwa pointi chache.

AZAM FC hawatanii buana! hivyo ndio unaweza kusema baada ya uongozi wa timu hiyo kuamua kutoa motisha kwa mastaa wao kupambana kumaliza nafasi ya pili kwa ahadi ya kuwapa zawadi ya fedha Sh300 milioni inayotolewa kwa mshindi wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Ahadi hiyo imetolewa ikiwa ni siku moja kabla ya timu hizo mbili kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa kesho, jijini Dar es Salaam, ambapo timu hizo mbili zinachuana kuwania nafasi ya pili, hivyo mkwanja huo umewekwa kuhakikisha kwamba Mnyama hatoboi.

Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 25 ikishinda 17, imetoka sare mechi sita na kupoteza michezo miwili wamekusanya pointi 57 wakiiacha nyuma kwa pointi nne Simba ambayo wanashindania nafasi hiyo kulingana na kuachana kwa pointi chache.

Simba ipo katika nafasi ya tatu ikiwa imecheza mechi 24, nyuma mchezo mmoja na washindani wao hao ambao wana kiporo cha mchezo mmoja wakiwa  wameshinda mechi 16, sare tano na kufungwa tatu wakikusanya pointi 53.

Timu hizo kesho zitakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo, na Mwanaspoti limepata za ndaaani kabisa kuwa uongozi wa timu chini ya Yusuf Bakhresa umewaahidi wachezaji kuwa endapo watamaliza nafasi ya pili watalamba Sh300 milioni ambayo ni zawadi ya mshindi wa pili.

"Kiuongozi amewaambia wachezaji wanatakiwa kupambana ili waweze kumaliza nafasi ya pili na kama watafanikisha hilo basi zawadi ya fedha ya mshindi wa pili itakuwa ya kwao," kilisema chanzo hicho chetu.

"Ushindani ni mkubwa na malengo yalikuwa kutwaa taji tumeteleza sasa mapambano ni kuhakikisha tunamaliza nafasi ya pili hilo litachochewa nguvu na ahadi iliyotolewa na viongozi wa juu." 

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi ilibainisha kuwa bingwa ametengewa Sh100 milioni kutoka Benki ya NBC na Sh500 milioni kutoka Azam.

Ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kassongo amesema mshindi wa pili ataondoka na Sh50 milioni kutoka NBC na Sh250 milioni kutoka Azam.

“Wa tatu atazawadiwa Sh30 milioni kutoka kwa mdhamini wa Ligi, lakini pia 225 kutoka Azam,” amesema.