Yanga v Simba katika jicho la mwewe

Monday February 18 2019

 

By Edo Kumwembe

WALE mapacha wa Kariakoo walicheza juzi Jumamosi. Ilikuwa mechi tamu. Ilisisimua wengi na hapana shaka kuna mashabiki, hasa wa Simba watakuwa wamejifunza kitu baada ya mechi ya juzi. Haikwenda kama walivyotaka.

Tuanze wapi? Tuanze na tukio la Ibrahim Ajibu kuwapa mikono wachezaji wake wakati mgeni wa heshima, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri Harrison Mwakyembe akikagua timu zote mbili kabla ya kuanza kwa mechi. Kuna video inatembea mitandaoni ikimuonyesha Kelvin Yondani akigoma kutoa mkono kwa Ajibu.

Yondani alikuwa sahihi. Tangu lini nahodha akawapa mikono wachezaji wake wakati mgeni wa heshima akikagua timu? Kuna vitu vya kumuelekeza Ajibu katika majukumu yake ya unahodha. Pale nahodha alipaswa kuwatambulisha wachezaji wake sio kuwasalimia.

Kuhusu mechi yenyewe ukweli ni kwamba Yanga inapaswa kupongezwa na mashabiki wake kwa kupambana na Simba. Sijui ilikosea wapi mechi ya raundi ya kwanza. Hii ilikuwa mechi tofauti kabisa.

Mechi ya kwanza ilipatwa na kiwewe. Ilikuwa inahamisha mipira ovyo. Inabutua. Mechi hii Yanga iliweka mpira chini na hivyo kuipa Simba kazi ya kukaba vilevile. Mechi ya kwanza ilikuwa ina njia moja tu, ya Yanga kuikaba Simba.

Kifupi ilijaribu kupishana. Fei Toto aliituliza timu wakati ikiwa na mpira katika eneo lake. Ikajaribu kupita katika njia za mpira mpaka katika lango la Simba. Ilipata nafasi kadhaa tofauti na pambano la kwanza. Ilipata kona kadhaa. Iliilazimisha Simba kucheza faulo kadhaa.

Ilikuja kufungwa kipindi cha pili. Na nani? Meddie Kagere. Nilikuwa natazama mechi katika televisheni mkoani Mtwara. Shabiki mmoja wa Yanga alikuwa anamponda Kagere kuwa alikuwa amedhibitiwa sana na mabeki wa Yanga. Nikamwambia atamuona Kagere wakati anashangilia tu.

Ni kweli. Kama ilivyokuwa katika pambano dhidi ya Al Ahly ndivyo ilivyokuwa katika pambano la juzi Jumamosi. Kagere hakuonekana mpaka wakati anashangilia. Kagere ana sifa zote za mshambuliaji. Anajua kujipanga. Kuna wakati haonekani mchezoni lakini anajua maeneo ambayo mpira utaangukia katika boksi la timu pinzani. Anahitaji nafasi moja tu kufunga. Ndicho alichofanya.

Simba ilikuwa timu bora uwanjani, Yanga ilikuwa wapinzani bora uwanjani. Mashabiki wa Yanga ambao wengi wao walikacha kwenda uwanjani nadhani watakuwa wanajuta kwa sababu hawakutazamia kama timu yao ingekuwa wapinzani bora uwanjani.

Kulikuwa na mpango wa Simba kuifunga Yanga mabao mengi. Wazo zuri lakini siku nyingine nadhani mashabiki na viongozi wa Simba waliendeshe kimya kimya tu jambo hilo. Wale wachezaji wa Yanga nao ni wanaume ambao huwa wanahisi fedhea.

Walijua kilichopangwa na Simba nadhani wakajiandaa. Hata katika benchi lao asingekuwepo kocha wasingeukubali mpango wa Simba.

Hofu kubwa ilikuwa upande wa kipa, Ramadhani Kabwili lakini Simba haikumfikia mara nyingi kama ambavyo mara ya mwisho ilimfikia Beno Kakolanya mara nyingi zaidi. Kulikuwa na hofu huenda Simba ingerudisha mabao iliyofungwa dhidi ya Al Ahly ugenini lakini haikutokea kwa sababu Yanga ilikuwa na nidhamu katika ulinzi na viungo wake waliisaidia safu ya ulinzi.

Kulikuwa na tatizo jingine katika mechi.

Clataous Chama mbona anapotea kila mechi kubwa siku za karibuni? Chama huyu sio yule wa Mbabane. Sasa hivi imekuwa mazoea anatoka Chama anaingia Hassan Dilunga. Ile mechi dhidi ya Nkana alitoka mtu mwingine akaingia Dilunga kwenda kushirikiana na Chama na Simba ikapata bao. Sasa hivi wanapishana.

Hofu yangu ni rekodi na historia ya soka letu. Mastaa wa kigeni wanakuja na moto mkubwa halafu wanapotea kadiri mechi inavyokwenda. Hata Papy Tshishimbi alikuja na moto mkubwa halafu akapotea. Sasa hivi anajikusanya upya.

Kuna mengi yalitokea lakini nimefurahishwa na jinsi ambavyo mashabiki wa pande zote mbili walivyoridhishwa na matokeo. Inatokea mara chache. Yanga walifurahishwa na kile walichokiona kutoka kwa timu yao, Simba walifurahishwa na ushindi kama ilivyo ada kwa ushindi wowote ule wa mechi ya mtani wa jadi.

Mwisho kabisa niwapongeze watu watatu. Yule beki wa kulia wa Yanga, Paulo Godfrey ni kijana ambaye atakuja kulisaidia taifa baadaye. Ana kasi nzuri uwanjani. Anajiamini. Kucheza mechi za Simba na Yanga kwa kiwango kile cha kujiamini anastahili pongezi.

Halafu Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anazidi kurudi vizuri. Nadhani amesahau majeraha yake na amesahau benchi la muda mrefu aliloipigwa na Asante Kwasi. Nadhani anahitajika katika kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza dhidi ya Uganda mwezi ujao.

Mwisho kabisa ni kwa mwamuzi wa mechi, Hans Mabena. Alitulia na kuchezesha vizuri. Makosa madogo madogo kutoka kwake yalikuwa ya kibinadamu zaidi. Kwa umri wake wa miaka 28 kuchezesha mechi kama ile nadhani anastahili pongezi. Wachezaji pia walimsaidia kwa sababu walitaka kuonyeshana ujuzi.