Wababe wa Kiingereza walivyokuzwa na West Ham United utotoni

Muktasari:

  • West Ham United kwa miaka mingi imekuwa ni shule ya kuibua vipaji vya nyota wengi wanaotamba England na duniani, lakini wameshindwa kuisaidia timu hiyo kurudi katika ubora wake wa mwanzoni mwa miaka ya tisini

USIIDHARAU sana klabu inayoitwa West Ham United. Hata kama haina mafanikio katika soka la Kiingereza lakini inabakia kuwa klabu ya Kiingereza ambayo imewaibulia Waingereza mastaa wengi waliotamba katika kizazi ambacho kwa sasa kinaishia.

Michael Carrick – (1999-2004)

Michael Carrick ni mmoja kati ya viungo wachache, ambao ulimwengu wa soka umegoma kuwapa heshima inayowastahili. Kiungo huyo mkabaji wa kati ni aina ya viungo wanaojua kutumia akili uwanjani kuliko nguvu.

Ana uelewewa mzuri wa kuusoma mchezo, kupiga pasi, kukaba na kufunga mabao mara chache chache, ni baadhi ya sifa zilizomsaidia kutengeneza kombinesheni matata na Paul Scholes, pale Old Trafford na kumbeba katikati ya kundi la viungo wenzake.

Kitu ambacho wengi hawafakihamu ni kuwa, Carrick ni mmoja kati ya mazao ya klabu ya West Ham. Alilelewa na kupikwa klabuni hapo kwa miaka saba. Hata wakati West Ham, ikishuka daraja (2003), Carrick hakuondoka.

Baadaye alijiunga na Tottenham, kabla ya kutua Old Trafford mwaka 2007 ambapo alitamba klabuni hapo na sasa ni kocha msaidizi wa Mreno, Jose Mourinho.

Joe Cole (1998-2003, 2013-14)

Majeraha yalimzuia kupata mafanikio ambayo wengi walitarajia atayapata.

Hata hivyo, alichokifanya Joe Cole katika miaka yake saba aliyokaa pale Stamford Bridge si haba. Cole, mmoja kati ya wachezaji wa Kiingereza wenye vipaji vya hali ya juu aliibuliwa na West Ham kuanzia mwaka 1998 alipotinga katika kikosi cha kwanza hadi mwaka 2003.

Baada ya kuiva akaibukia klabu nyingine kama Chelsea na Liverpool lakini akarudi tena klabuni hapo msimu wa 2013-2014. Akaendelea kucheza kwingine kama kama vile Aston Villa lakini mapema wiki hii ametangaza rasmi kuachana na soka akiwa na umri wa miaka 37. Hapana shaka kwa yote aliyoyafanya katika soka na kufanikiwa atakuwa anaishukuru sana West Ham iliyomuibua.

Jermain Defoe (1999-2004)

Staa mwingine wa England ambaye kipaji chake kiliibuliwa na West Ham jijini London. Defoe ameichezea Tottenham kwa vipindi vitatu tofauti lakini ni West Ham ndiyo iliyomuweka katika chati. Aliyembeba sana katika maisha yake ya soka ni kocha wa zamani wa timu hiyo, Harry Redknapp.

Na kocha huyo ndiye ambaye alikuwa anazurura na Defoe katika klabu mbalimbali baada ya kukiamini kipaji chake tangu akiwa mdogo pale West Ham. Amezurura klabu nyingine za Portsmouth, Toronto FC (Marekani), Sunderland na Bournemouth ambayo anaichezea mpaka sasa lakini ni West Ham ndiyo iliyomuibua.

Rio Ferdinand (1995-2000)

Mmoja kati ya mabeki bora wa muda wote Manchester United na England. kwa muda mrefu chini ya Kocha Sir Alex Ferguson alitengeneza safu imara ya ulinzi Old Trafford akiwa na mbabe wa Serbia, Nemanja Vidic.

Msingi wa uimara wake ulianzia West Ham akiwa kinda kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2000 alipojiunga na Leeds United kwa rekodi ya uhamisho ya dunia kwa upande wa mabeki. Alinunuliwa kwa dau la Pauni 30 milioni. Misimu miwili baadaye akaivunja tena rekodi hiyo kwa kutua Manchester United.

Paul Ince (1986-1989)

Chanzo cha ufalme wa Paul Ince, kiungo aliyezichezea klabu tatu kubwa, barani Ulaya, katika miaka ile ya 80 (Manchester United, Inter Milan na Liverpool), kilikuwa ni klabu ya West Ham. Ince alitokea katika mikono ya wagonga nyundo hao wa Jiji la London na kujiunga na United katika dili lililozua gumzo kubwa barani Ulaya. Miaka yake saba ya kukaa Old Trafford ilimshuhudia akifunga mabao mengi na kuwapa Masheatani Wekundu kiburi kwenye Ligi Kuu ya England. Baadaye alihamia Inter Milan lakini akawashangaza wengi alipoamua kurudi nyumbani akatua kwa wapinzani wakubwa wa Manchester United, Liverpool. Akiwa na Manchester United kisha Liverpool, Ince mara zote alikuwa akikumbana na wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa West Ham pindi alipokwenda kucheza katika Uwanja wa Upton Park kutokana na kuzomewa mara kwa mara. Mashabiki hao walikerwa na jinsi alivyoihama West Ham wakati anakwenda Old Trafford.

Glen Johnson (2002-2003)

Msimu wake mmoja tu kutoka katika timu ya vijana na kupata nafasi katika kikosi cha wakubwa ulitosha kumpa dili nje ya West Ham.

Alikuzwa pale akiwa kinda lakini katika msimu wa kwanza tu alitinga kikosi cha kwanza na Chelsea ilimuona na kumvuta Stamford Bridge. Hakupata nafasi sana Chelsea lakini baadaye akatamba na Liverpool kisha Portsmouth kabla ya kumalizia maisha yake ya soka akiwa na Stoke City kwa sasa.

Frank Lampard (1995-2001)

Ni mmoja kati ya viungo bora wa enzi zake na mmoja kati ya watu walioipa Chelsea kiburi katika ulimwengu wa soka.

Muingereza, Lampard hahitaji utambulisho. Alichokifanya kinatosha kumtambulisha. Mkali huyo wa kupiga mashuti na kufunga mabao muhimu, aliandaliwa pale West Ham kuanzia mwaka 1995 hadi 2001.

Ni Chelsea ndipo alikoweka alama zaidi baada ya kuibuka kuwa mfungaji bora wa muda wote klabuni hapo ingawa nafasi yake ni kiungo mshambuliaji. Licha ya baadaye kuzurura kidogo Manchester City na New York City FC lakini Lampard anakumbukwa kwa kuanzisha makali yake West Ham chini ya Kocha Redknapp. Kwa sasa ni kocha wa Derby County ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mark Noble (2004-mpaka sasa)

Injini ya West Ham ambayo inaunguruma mpaka sasa katika jezi ya rangi ya wababe hawa wa London.

Noble alianza kukichezea kikosi cha West Ham tangu akiwa kijana na aliingia katika kikosi cha kwanza mwaka 2004 na amekuwa klabuni hapo mpaka sasa ingawa aliwahi kupelekwa kwa mkopo katika klabu za Hull City na Ipswich Town wakati akianza kukomaa.

Kama vile kulipa fadhila kwa klabu hii, Noble amekuwa pia akihusishwa na klabu katika programu mbalimbali za kukuza makinda klabuni hapo.

John Terry (1991-1995)

Wengi wanadhani historia ya John Terry inaanzia Chelsea na kuishia Chelsea.

Hilo sio sahihi. Terry aliibukia West Ham akiwa na umri wa miaka tisa kabla ya kwenda Chelsea akiwa na umri wa miaka 14, mwaka 1999.

Tofauti na mastaa wengine walio katika orodha hii Terry hakuwahi kugusa katika kikosi cha kwanza cha West Ham kwa sababu alikuwa mdogo zaidi lakini ukweli West Ham ndio iliyokiona kipaji chake katika mitaa ya London ya kuamua kukilea kabla hajaibukia Stamford Bridge ambako aliweka heshima kubwa akiwa nahodha wa Chelsea pamoja na Timu ya Taifa ya England kwa wakati mmoja.