NYUMA YA PAZIA: Sadio Mane anahitaji kunyanyua mguu tena?

UNAKUMBUKA siku ya mwisho kutazama mpira live mbele ya televisheni yako ilikuwa lini? Sio kazi rahisi. Inaonekana kama miaka mingi sasa. Lakini kumbe dunia inaweza kuendelea. Badala ya kujadili mechi ya jana au ya kesho sasa tunajadili mijadala.

Kwa mfano. Juzi Diomansy Kamara amefungua mdomo wake kuanzisha mjadala. Unamkumbuka Diomansy? Bishoo mmoja wa Kisenegal aliyewahi kucheza London. Alicheza Fulham. Akafungafunga mabao akatokomea zake kusikojulikana.

Diomansy amedai staa mwenzake wa Senegal, Sadio Mane anahitaji kuhama Liverpool na kwenda Real Madrid au Barcelona kwa ajili ya kutwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, Ballon d’Or. Ni kweli? Hapana. Sidhani.

Unahitajika wehu kumnyima staa mkubwa wa Liverpool taji la mwanasoka bora wa dunia baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kupungua makali yao. Kabla ya Ronaldo na Messi kuanza kupokezana tuzo kwa miaka 10, mchezaji wa mwisho kutwaa tuzo hiyo alikuwa Ricardo Kaka akiwa Italia na AC Milan.

Baada ya Ronaldo na Messi kupokezana kwa muda mrefu, mchezaji ambaye alikuja kuvunja utawala wao alikuwa ni Luka Modric mwaka 2018. Sawa, kwanini Luka? Kwa sababu alikuwa ametwaa ubingwa wa Ulaya na Real Madrid lakini pia ulikuwa mwaka wa Kombe la Dunia na Croatia yake ilifika fainali. Messi na Ronaldo hawakuambulia chochote katika michuano hiyo.

Watu waliokariri kuwapatia tuzo Messi na Ronaldo walifanikiwa kupata upenyo wa kuwaondoa kwa muda na kumpa Luka. Msimu mmoja baadaye Messi alirudi tena katika utawala wake. Wengi walishangaa kwanini isiwe staa yeyote kutoka Liverpool baada ya kuvuna taji la Ulaya mwaka jana.

Tunarudi kwa Diomansy. Alichosema kina ukweli? Sidhani. Baada ya Ronaldo kuondoka Real Madrid kuna mchezaji gani aliyemuacha ambaye ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo? Baada ya Lionel Messi kuelekea katika siku za mwisho za usakataji wake, mchezaji gani mwingine wa Barcelona ambaye ana nafasi hiyo? Simuoni.

Dunia inasubiri Kylian Mbappe aende Real Madrid na kutwaa tuzo kubwa ili apewe tuzo hiyo. Dunia pia inasubiri Neymar arudi Barcelona afanye mambo makubwa na kupewa tuzo hiyo. Lakini ukichunguza sana yote haya sio lazima. Sio lazima kwa Mbappe kwenda Madrid kisha akawa Ronaldo mpya. Kuna Ronaldo mmoja tu. Lakini sio lazima kwa Neymar arudi Barcelona na kufanya mambo makubwa ili apewe tuzo hiyo. Sio lazima.

Wote tumeona jinsi ambavyo maisha ya soka ya Neymar yalivyokwama. Lakini tujikumbushe kuna Messi mmoja tu kama ambavyo kuna Ronaldo mmoja tu. Tusizungumze habari za warithi wao katika klabu hizi.

Ni nyakati kama hizi basi Mane anaweza kuwa mwanasoka bora wa dunia akiwa na Liverpool tu. Kitu cha msingi ni kuendelea kufanya maajabu anayofanya. Tatizo lake na la timu ni kama hili la kuruhusu ubingwa wa Ulaya uwapite baada ya kutolewa na Atletico Madrid.

Kama Mane akiendelea kufanya maajabu na Liverpool anaweza kupewa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia akiwa pale pale Anfield. Nje ya Ronaldo na Messi, Real Madrid na Barcelona ni timu za kawaida. Hazipo katika kiwango cha Liverpool.

Nyakati pekee ambazo zingekuwa ngumu kwa Mane basi ni wakati ule Pep Guardiola akiwa na Barcelona.

Nyakati zile kuna wanasoka wengi zaidi waliostahili kuwa wanasoka bora wa dunia nje ya Messi na Ronaldo lakini hawakupewa tuzo. Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Wesley Sneijder waliwahi kustahili sana lakini wakakutana na vigingi vya Messi na Ronaldo.

Kwa sasa Barcelona haina Iniesta. Hata ukiamua kumtafuta mchezaji mwingine wa Barcelona wa kuchukua tuzo nje ya Messi hauwezi kumuona. Inabidi ufanye kazi ngumu ya kuidanganya duniani. Vinginevyo unaweza kueleweka ukimpa tuzo Mane.

Sababu kubwa inayoweza kumpeleka Mane Barcelona au Real Madrid kwa sasa, hasa Madrid, ni kukamilisha maandiko tu. Real Madrid ni klabu kubwa zaidi duniani. Hakuna ubishi katika hili. Hauwezi kuilinganisha na Liverpool.

Real Madrid ni timu ambayo kila mchezaji anaota kuichezea. Barcelona nayo pia ipo katika mkumbo huu. Kwa sababu hii Mane anaweza kwenda moja kati ya klabu hizi za Hispania ingawa kwa bahati mbaya au nzuri wachezaji wa Afrika hawaoti sana kuzichezea klabu hizi kama wale wa Amerika Kusini.

Na bahati mbaya nyingine ni kwamba ni wachezaji wachache sana kutoka Afrika wamewahi kupata mafanikio makubwa katika klabu hizi. Utamkumbuka Samuel Eto’oo tu lakini wengine walicheza katika mafanikio ya kawaida.

Labda na Geremi Njitap.

Madrid na Barcelona ni ngazi za mwisho kabisa katika soka na kabla ya hapo ilikuwepo AC Milan. Lakini kwa upepo unavyovuma sasa ni wazi kwamba Mane anaweza kupata taji lake akiwa Anfield tofauti na Kamara anavyofikiria.

Tunakoelekea ni wazi kwamba mwanasoka bora wa dunia anaweza kutoka nje ya njia za Real Madrid na Barcelona kama ilivyokuwa kabla ya utawala wa Messi na Ronaldo kule Hispania. Ikumbukwe kabla ya hapo Kaka alitwaa alitwaa akiwa Italia na Ronaldo alitwaa akiwa Manchester.