Mgosi awapa ukweli Ajibu, Said Ndemla-2

JANA kwenye sehemu ya kwanza Musa Mgosi mchezaji wa zamani wa Simba alitueleza mambo mbalimbali ya kuvutia ikiwemo jinsi Luis Jose anavyoitendea haki jezi yake ndani ya Msimbazi kwasasa.

Hebu endelea kumsoma ni miongoni mwa wachezaji ambao wamepata heshima ndani ya Simba kama ilivyo kwa Seleman Matola kaichezea na sasa ni kocha msaidizi wa timu hiyo.

Mgosi aliichezea kwa mafanikio makubwa, baada ya kustafu akapewa cheo cha meneja, akapewa dhamana ya kuifundisha Simba B na sasa kocha mkuu wa Simba Queens.

Anasema ameendelea kupata uzoefu kupitia majukumu aliyopewa. “Niliweza kufanya kwa ustadi nikiwa meneja, nikapewa majukumu mengi ya kocha Simba B na sasa nipo na timu ya wanawake,” anasema.

KADI TATU NYEKUNDU

Anasema tangu aanze kucheza Ligi Kuu mwaka 2002 amepata kadi nyekundu tatu, moja akiwa Mtibwa Sugar na mbili akiwa na Simba.

KIKOSI ANACHOKIKUBALI

Anasema kuna vikosi bora vingi kwake ndani ya Simba akiacha mbali kile kilichofika robo fainali ya CAF cha mwaka 2003, amekitaja cha msimu wa 2008/09 ambacho kilichukua ubingwa bila kufungwa.

Anasema kipa alikuwa Juma Kaseja, Said Swedi, Soud Abdallah, Kelvin Yondani, Juma Nyoso, Jerry Santo, Nico Nyagawa, Mohammed Banka, Seleman Ndikumana, Mussa Hassan Mgosi na Ulimboka Mwakingwe.

KOCHA BORA KWAKE.

Anamtaja Kocha Mzambia Patrick Phiri kwamba alijua namna ya kuwajenga wachezaji, kuna wakati alikuwa rafiki na baba.

Anatoboa siri kwamba katika kazi anayofanya kwa sasa alijifunza mengi kwake na yanamsaidia kukaa vizuri na wachezaji.

KAMA SIO SOKA ANGEKUWA INJINIA

Anasema kujikita na soka kumeibukia njiani, kazi aliyokuwa anaipenda na ilikuwa damuni ni ufundi magari na kwamba alikuwa akitoka shule anaenda gereji kisha mazoezini.

“Ndoto yangu ilikuwa kuwa fundi gereji licha ya kwamba nilikuwa naupiga mwingi, lakini Mungu ana mipango yake nipo kwenye soka ila pia naweza nikatengeneza gari vizuri tu,” anasema.

SOKA LIMEMLIPA

“Silipi kodi kwani naishi kwangu, nasomesha watoto, vingine siwezi kuweka wazi sana,” anasema.

Anasema gari yake ya kwanza kulitumia ilikuwa Toyota Grand alinunua 8 milioni ilikuwa mwaka 2006.

“Nilikuwa na Toyota Grand enzi hizo wanasema mchezaji ana gari, Ila kwa sasa natumia Benzi, simu nilianza na Nokia zile ambazo zilikaa engo tatu ila kwa sasa natumia Iphone,” anasema ana tasisi yake ya soka inayoitwa Mgosi Football Academy ina wachezaji 35 kuanzia umri wa miaka 17 mpaka 22.

“Malengo yangu ni kukuza vijana katika misingi ya mpira, kufundishwa mpira, kufanikisha ndoto zao kupitia vipaji vyao kisha kuwafanyia mpango wa kupata timu hapa na nje,” anasema.

“Nategemea soka linifanyie mengi, napambana na ipo siku ndoto yangu itatimia na kuendelea kuwa mfano kwa wengine,” anasema.

AJIBU, KICHUYA NA NDEMLA

Anawatazama kama vijana wenye uwezo mkubwa. Ushauri wake anawataka wapende kujifunza kujua na sio wajione wanajua.

“Mtu yeyote akifikia hatua ya kujua basi ujue ndio mwisho wake hawezi kuendelea na safari, kwani hataweza kupokea vitu vipya, wadogo zangu waanze moja, kujifunza na watanawiri kwenye soka bado wana muda wa kufanya maajabu,” anasema.

“Nakumbuka wakati nacheza nilikuwa nikikaa nje basi nilikuwa najisikia vibaya naona napoteza pesa maana ukicheza ndio unaonekana,” anasema.

Anasema wachezaji matajiri duniani kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanafanya mazoezi kama punda je, mastaa wanaojiendekeza kwa uvivu wao ni nani mpaka wavimbe vichwa.

“Wanaitwa majina mazuri kwa sababu ya kazi nje na hapo hakuna thamani kabisa, wajitambue waweke kando ustaa wajitume watafika,” anasema.

SIMBA QUEENS

Anasema kuna tofauti kubwa kati ya soka la wanawake na wanaume na ameweza kumudu kukaa nao vyema.

“Wanaume ni wepesi wa kushika ukiwafundisha vitu lakini uwanjani sio watendaji, wanatumia asilimia 20 za maelekezo 80 wanafanya yao ndio maana makocha wanalalamika.

“Wanawake wanatumia asilimia 80 na 20 wanafanya yao na wepesi kushika maelekezo na kwamba wana hamu ya kuonyesha vipaji vyao,” anasema.

KWA NINI SIMBA QUEENS

“Hilo limefanikiwa kwa sasa nawajengea wajitambue wao ni kina nani, thamani yao, kufanya maendeleo na kuwa na chaguzi nzuri na wenza wao.

“Uzuri wa kikosi cha Simba tuna matroni mwanamke na daktari mwanamke, hivyo wanakuwa wanatusaidia kuwafunza uhalisia wa maisha,” anasema.

VISHAWISHI VYA WAREMBO HAO

Anasema jambo la kwanza ana mke anayempenda sana, pia hajazidisha mazoea kwamba wakati wa kazi hataki utani.

“Malengo yetu ni ubingwa hivyo siwezi kuleta mzaha na kazi, wananiona ni baba, kaka, kocha na rafiki nimechukua mifumo ya Kocha Phiri, fanya utafiti uliza utapata ukweli wa hiki ninachosema,” anasema.

WAMEZALIWA 12

Ni mtoto wa tisa kati ya 12 aliyozaliwa nao, asilimia kubwa ni wanasoka wakiongozwa na baba yao aliyekuwa kipa wa Coastal Union na African Sports zamani.

Mzaliwa wa kwanza kwao ni Athuman, Bakari, Ramadhan, Omary, Idd, Amina, Khatibu, Mariamu ambaye ni marehemu yeye, Juma, Ally na Kassim.

“Familia yangu kwa asilimia kubwa ndio iliyonivutia kuwa mwanasoka nikianzia na baba yangu alikuwa kipa wa Coastal Union na African Sports,”

“Kaka angu Athuman, Bakari sijawashuhudia wakicheza bali Ramadhan, Omary na Idd wamecheza sana timu za mkoa na walikuwa na uwezo mkubwa zaidi,”amesema.

FAMILIA YAKE

Ana mke mmoja na watoto watatu wa kwanza ni Hassa (16) yupo kidato cha nne, Nairati (12) anasoma darasa la sita na Naifati (4 kasoro) anasoma chekechea.

“Mke wangu sikukutana naye mazingira ya mpira, wakati nikiwa kidato cha pili yeye alikuwa kidato cha kwanza, mimi nilikuwa nakaa shule yeye anatokea nyumbani.

“Uhusiano wetu ulikuwa mazito na yakweli kwani alikuwa ananifungia chapati, vitumbua nikichoka kula msosi wa shule, alinifanya niwe na malengo ya maisha ya baadaye, ndio maana unaona tumedumu mpala leo,” anasema.

Anasema tangu wafunge ndoa mwaka 2006 mapenzi yao yamekuwa yanaongezeka siku hadi siku.

WACHEZAJI NA MAHUSIANO

“Ogopa mwanamke anakubali kuwa na wewe kisa umarufu kuna wakati unaweza ukaisha ama pesa zikaisha hapo ndipo mambo yanakuwa yanabadilika, kama alivifuata hivyo atakwenda kwa mwingine.

“Mchumba wangu alinisaidia kuwa na msimamo kwani ni mwanamke ambaye alikuwa ananisaidia kufikiria zaidi kesho na sio leo na ndio maana ndoa yangu haijayumba,”anasema Mgosi ambaye mwanaye mkubwa ana kipaji cha hali ya juu na anacheza namba sita na nane na kwamba amejaribu kumzuia ili asome anaona kama anataka kugonga mwamba.

“Anacheza timu za shule, kuna wakati namzuia asiende kucheza mtaani, wenzake wanaandamana kuja kumuomba nyumbani nakuwa nashindwa cha kumfanya namwacha aende.

“Wakati wa mapumziko huwa nafanya naye mazoezi nakuwa namwelekeza nini chakufanya kimbinu,naamini miaka inayo kila mtu atajua uwezo wake, ingawa kwa sasa namsisitiza umuhimu wa elimu,” anasema. Mgosi ambaye alianzia soka kwenye mashindano ya shule za msingi (Umitashumta) ambayo yalifanyika Iringa mwaka 1997 akiwa darasa la saba, Idd Kipingu aliona kipaji chake.

“Kama unavyojua vipaji vilikuwa vingi chini ya Kipingu katika Sekondari ya Makongo, wakati nacheza mashindano mbalimbali Simba, JKT Tanzania kipindi hicho ilikuwa JKT Ruvu na Mtibwa Sugar ziliniona,” anasema.

“Kilichowavutia zaidi ni baada ya kuichezea Timu ya Taifa ya Vijana U-17 nikitokea Makongo, Ila sikutaka niikubalie Simba wala Mtibwa wakati huo, niliangalia umri wangu na watu waliopo kwenye timu hizo na uwezo wao.

“Mwaka 2002/03 ndipo niliposaini mwaka mmoja na JKT Tanzania sababu kubwa ilikuwa inaendana mazingira ya kijeshi na Makongo nilipokuwa nasoma na ilikuwa jirani na shule,” anasema.

ALIVYOTOROKA JESHINI

Anasema wakati anaendelea na soka, huku anasoma shule alipelekwa jeshi akasoma kozi ya miezi mitatu kisha akarudi kuendelea na mishe zake.

Baadaye tena akapelekwa kusoma kozi ya pili kwa muda wa miezi sita ilipofika hatua ya kwenda kusoma ya tatu akabadili gia angani.

Mwaka 2003/04 Mgosi anasema jeshini walitangaza namba yake ya ajira na kituo cha kwenda kufanyia kazi lakini ilikuwa imebakia kozi ya mwisho.

“Zilikuwa zimebaki siku tatu kwenda kwenye kozi, nilipoona Mtibwa Sugar na Simba bado wananifuatilia nikaamua kutorokea Morogoro, wacha nitafutwe na makamanda.

“Nilipoona mambo magumu ni pale nilipopigiwa simu na vigogo wa juu, ikabidi niwaeleze ukweli kwamba nipo na Mtibwa Sugar naomba waniruhusu niendelee na soka. Yakawekwa makubaliano ambayo ni ya siri hayafai kuyazungumza hapa,” anasema. Anaendelea kusimulia kwamba akasaini Mtibwa Sugar msimu mmoja kwa dau la 1.4 milioni.

“Hiyo pesa nilitumia kununulia vitu vya ndani kama sofa, kifupi geto likawa fulu ili mchumba wangu akija anione bonge la bwana. Pia nilikuwa napenda nikutane naye kwangu na sio hoteli tena,”

“Pia, nilimgawia baba yangu Hassan, Sh 200,000 na mama yangu Fatuma nikampa kiasi kama hicho, nikapewa baraka zote, mchumba wangu nikampiga pamba basi maisha yakaendelea,” anasema.

Simba ilihitaji huduma yake msimu uliofuata akaona asichezee bahati akakubali kusaini 2004 ndipo mambo yalipoanza kunoga.