MAONI YA MHARIRI: Klabu zisajili wachezaji wa kuzibeba anga la kimataifa sio Ligi Kuu pekee

LIGI Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni kwa sasa kukiwa na mchuano wa ubingwa ulio kwa klabu tatu za Yanga, Simba na Azam FC, huku vita nyingine ikiwa mkiani kwa klabu zinazopambana kuepuka kushuka daraja.

Ingawa mfumo wa sasa wa ligi unaoshirikisha klabu 20 upo tofauti ambapo kuna timu mbili za Ligi Kuu za mkiani zitachuana na klabu nyingine mbili zitakazoshika nafasi ya juu baada ya zile mbili za awali kupanda Ligi Kuu msimu ujao zitacheza kuwania nafasi moja ya kupanda, lakini kazi bado mbichi.

Katikati ya ligi kuelekea ukingoni, baadhi ya klabu kwa sasa akili zao ni kuhusu usajili wa nyota wapya kwa nia ya kuimarisha vikosi vyao, kulingana na nafasi walizonazo ndani ya ligi inayomalizika.

Tumeanza kusikia Azam wakiwasainisha baadhi ya nyota wao waliokuwa wakimaliza mikataba kwa nia ya kuwabakisha, huku klabu za Simba na Yanga zikihusishwa na wachezaji wa ndani na nje ya nchi ambao inawataka kwa msimu ujao. Siko kitu cha ajabu kinachofanyika kwa klabu hizo. Hii ni sehemu ya maandalizi ya timu inayojielewa na iliyo na mipango madhubuti ya kufanya vyema.

Wakati klabu zikianza michakato ya kusajili wachezaji wapya wa ndani na nje ya nchi ni vyema kama wadau wa michezo kuzikumbusha klabu hizo zifanye usajili wao kwa umakini mkubwa.

Lazima zisajili wachezaji ambao watakuwa na manufaa kwao katika ligi ya ndani na nje ya nchi kwa maana ile ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Klabu hizo kubwa za juu zinazopambania ubingwa kwa sasa bila shaka wameshanusa harufu ya kupata tiketi ya kimataifa kwa msimu ujao.

Umuhimu wa wachezaji bora tumeona unavyovisaidia baadhi ya klabu barani Afrika na hata hapa nyumbani Simba, Yanga na Azam zimekuwa zikitamba kwa vile zimekuwa zikisajili vyema, lakini bado wanapaswa kuongeza umakini zaidi.

Kwa mfano katrika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imefika robo fainali kwa vile baadhi ya nyota wake wa kigeni na hata wa wa ndani walikuwa na ubora uliowasaidia kuchuana na wenzao wa klabu nyingine.

Meddie Kagere aliyeibuka mfungaji bora wa Simba kwenye michuano hiyo, Clatous Chama, John Bocco, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Aishi Manula, Emmanuel Okwi ni kati ya mifano ya usajili wa kujivunia wa Msimbazi.

Hata kwa Yanga leo imekuwa ikibebwa na kina Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko na wengine kwa sababu ni bora licha ya hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo Yanga. Kule Azam kina Tafadzwa Kutinyu, Donald Ngoma, Yakub Mohammed, Obrey Chirwa, Nicholas Wadada na Bruce Kangwa ni mifano ya usajili wenye akili.

Kwa kuwa tayari kuna baadhi ya majina yanayotajwa kumulikwa na mabosi wa klabu hizo, ingawa hatuna hakika kama walengwa ni mapendekezo ya makocha na mabenchi ya ufundi ya timu hizo ama ni utashi wa mabosi hao, lakini ni lazima klabu zifanye usajili kwa kuzingatia mafanikio zaidi.

Hata kama ni utashi wa mabosi wa klabu hizo, bado ni lazima kipaumbele chao kilenge zaidi kwenye ushiriki wao wa michuano ya kimataifa kuliko Ligi Kuu Bara ambayo kwa miaka mingi klabu hizo zimekuwa zikiitawala.

Simba na Yanga rekodi zao za ushiriki wa michuano ya kimataifa hazivutii hata kama zenyewe kwa zenyewe zimekuwa zikitambiana kwa rekodi za miaka ya nyuma.

Ukiondoa mafanikio ya msimu huu kimataifa, Simba imekuwa ikiitambia Yanga kuweza kucheza nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa) 1974 na kufika fainali ya michuano ya CAF mwaka 1993, lakini mafanikio hayo hayana maana kama taji halijafika nchini.

Yanga wenyewe ilikuwa ikitambia rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika robo fainali ya Klabu Bingwa mara mbili mfululizo mwaka 1969-70 na kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 na Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana ikiwa klabu pekee ya Tanzania.

Tambo hizo zinasaidia nini kama mataji ya michuano hiyo imechukuliwa na klabu nyingine? Ndio maana tunazikumbusha klabu hiyo kuchangamka sasa kwa kuhakikisha usajili wanaofanya unakuwa wenye malengo ya kimataifa.

Simba bila shaka imeona faida ya kyufanya usajili kwa umakini, hivyo wasirudie kilichowakuta miaka zaidi ya minne mfululizo ilipokuwa hawaiwakilishi nchi kwa kushindwa kuhimili vishindo vya wapinzani wao Yanga na Azam kiasi cha kupewa majina mabaya. Yanga kadhalika ni lazima ichangamke ili kuenda sambamba na changamoto za watani zao kwa kuonyeshana kazi na mwishowe mafanikio yao yaibebe Tanzania kwenye anga hiyo ya kimataifa.

Kama zitaendelea kufanya usajili wa kusaka sifa ama kutuliza mizuka ya mashabiki wao mitaani, lakini isilenge kusaka mafanikio anga za kimataifa, basi timu hizo zitarajie ziking’olewa na kuishia njiani tu.