Darasa anatuambia kama huna jipya kaa kimya

Monday November 5 2018

 

ZIPO sauti nyingi zinaulizia ukimya wa Darasa. Wanahoji mbona hatoi ngoma mpya? Sababu ya kuuliza hivyo ni kwa sababu kipo kipindi Darassa alilichukua soko la muziki Bongo na kuliweka mabegani kwake, kisha akaenda nalo mpaka maskani kwake Kiwalani, Dar.

Wimbo Muziki ulikuwa habari nyingine. Ulikuwa sawa na bondia wa uzito wa juu kwenye ulingo mmoja na mabondia wa uzani mwepesi. Muziki ulisababisha nyimbo nyingi kali zipepesuke. Darassa alifanya ubabe wa kiwango cha juu mno.

Wakati Muziki ukiwa wa moto sana, MwanaFA aliachia kitu kikali sana, Dume Suruali kwa ushirika na Vee Money. Matokeo ya jumla yakawa ni Dume Suruali kufurukuta lakini haukukaa palipostahili kutokana na thamani ya wimbo wenyewe.

Kwa sasa Darassa yupo kimya. Watu wanauliza mbona kimya kimezidi? Mapema wiki hii, mtangazaji na prodyuza wa vipindi, Clouds Media Group, Soud Brown, alinipigia simu ili kama mdau niweze kutoa maoni yangu kuhusu ukimya wa Darassa, je, faida ni nini na hasara ni ipi?

Nilimjibu Soud kuwa kama huna kitu cha kuongea ni vizuri ukae kimya kuliko kuongea pumba zitakazoshusha thamani yako. Hivyo ni sawa kwa Darassa kukaa kimya, kuliko kutoa wimbo ambao badala ya kumpandisha utamshusha.

Darassa alishaifikia pepo ya muziki wa kizazi kipya. Akawa namba moja. Anajua utamu wa mahali alipokuwa kipindi Muziki unafanya mabalaa yasiyozuilika sokoni. Kurejea kule inabidi awe na kazi yenye kuendana na soko. Hapaswi kukurupuka.

HASARA NA FAIDA

Tuje kwenye swali la msingi, ukimya wa Darassa una faida au hasara? Jawabu ni ndio kila upande. Zipo faida na hasara vilevile. Hata hivyo, hasara ipo karibu zaidi kuliko faida.

Tuanze na hasara; sauti nyingi zinazomuulizia Darassa zina maana kuwa anahitajika. Hii ni fursa kubwa kwake kwa sababu si kila wakati mwanamuziki anaweza kukaa kimya kisha watu wengi wakawa na shauku ya ujio wake. Hata sasa, wengi tu wapo kimya lakini hawauliziwi, ila Darassa anauliziwa.

Shauku hiyo ya watu juu ya ujio wa Darassa ni fursa kwake kama atatii kiu yao mapema. Kadiri anavyochelewa ndivyo na hamu ya watu kupokea kazi yake mpya inavyopungua. Kwa hiyo akichelewa sana, anaweza kutoa kazi kipindi ambacho watu hawatakuwa na mizuka naye.

Biashara ya muziki, nyimbo ndiyo bidhaa. Kanuni ya kibiashara ni ileile. Upatikanaji wa bidhaa hurahisisha mauzo. Wateja hawawezi kununua bidhaa isiyokuwepo au iliyo mbali. Hivyo, ili uuze bidhaa yako inatakiwa uhakikishe inakiwepo kwenye mzunguko. Unaweza kuitangaza sana bidhaa yako lakini sokoni haipo, hutauza.

Kwa maana hiyo, Darassa anavyokaa kimya, bidhaa zake zinakuwa hazipo kwenye mzunguko. Wakati huo, wengine wanatoa vyuma. Inabidi mashabiki wa Darassa wakumbatie wanamuziki waliopo wanaotoa madude. Kutahamaki, anaweza kuamua kurudi na kukuta ameshapoteza mashabiki lukuki.

Kuhusu faida; kukaa kimya ni dalili za kujipanga. Ni kipimo kwamba Darassa hakimbizwi na upepo wa soko (mainstream). Mwanamuziki anayepagawa kwa ajili ya mainstream, mara nyingi huweza kuharibu kazi kwa kulipualipua ili awahi kubamba sokoni. Ulipuaji wa kazi ni uharibifu wa kazi.

Muziki si sawa na maandazi au vitumbua, kusema kila siku utachoma na wateja watakuja kununua. Muziki huhitaji nafasi. Unatoa nafasi kwa mashabiki wasikilize kazi za wengine ili na wewe wakumisi. Ukiwa unatoa ngoma kila mara, hufika wakati hushtui tena. Mashabiki wanakuona wa kawaida. Usiniulize kwa nini Aslay kapwaya!

Darassa hatakiwi kupaniki kwa sababu anauliziwa sana. Ashushe presha, aendelee kujipanga. Wanaoulizia kazi yake mpya, ndio watakaoanza kuponda akitoa boko. Ajipange. Afanye utafiti. Ajiridhishe kitu cha kutoa kitakachoendana na wakati. Kama huna cha kuongea, bora ukae kimya kuliko kuongea pumba.

AKUMBUKE ALIPOTOKA

Nishike Mkono na Sikati Tamaa ni nyimbo bora zaidi siyo tu kuimbwa na Darassa bali pia katika soko la muziki Tanzania. Uzuri wa ujumbe na mashairi yake, ubora wa mistari yenye kufikirisha na floo nzuri ya Darassa, bado nyimbo hizo hazikumpa mafanikio.

Ukisikiliza mashairi ya Nishike Mkono na Sikati Tamaa, unapata picha kuwa Darassa alitumia akili nyingi kuandika, vilevile muda mrefu kutengeneza mitindo ya kufloo kutoka baa moja kwenda nyingine.

Wimbo Kama Utanipenda wa Darassa aliomshirikisha Rich Mavoko ulikuwa mzuri sana na ulimfungulia njia Darassa kuliko kazi zake za nyuma. Zile kazi za hisia na zenye kuufikirisha ubongo hazikufua dafu.

Darassa akazidi kunipa imani kuwa amefungua njia, kama alikuwa amefunikwa na paa basi limefunguka, ni pale alipotoa ngoma Too Much. Ni wimbo mkubwa lakini wa ujumbe wa moja kwa moja, siyo wa kuufikirisha ubongo.

Ukitaka kujua biashara ya muziki haipo ‘fea’, wimbo Muziki ndiyo ambao ulivunja miamba na kupasua anga la kibiashara na kumweka Darassa kwenye kilele chake. Muziki haukuwa wimbo wenye kuumiza sana kichwa, ila ulijaa misemo mitamu na ufundi wa prodyuza. Utamu wa wimbo ukawa haupingiki.

Baada ya kukaa kileleni na Muziki, Darassa alipaswa kutafakari kitu cha kumrejesha kwa kishindo, aliachia Hasara Roho ambao ni wimbo wa misemo kama Muziki, matokeo yake ukamfanya asiwe na jipya. Wimbo Utaniua ulivuja lakini haukujaa kishindo. Bora tu atulie ili akirudi awe amerudi kweli.