UKWELI NDIVYO ULIVYO: Kiki za wasanii wetu na maajabu ya KMC FC

Sunday February 24 2019

 

NI kweli dunia kwa zama hizi ni kama kijiji kimoja. Linalotokea kule, linafahamika fasta huku kiasi mtu haachwi nyuma kama ataamua tu kwenda na kasi ya utandawazi.

Teknolojia na mabadiliko yake yamerahisisha mambo, ndio kwa sasa kumekuwa rahisi tukio lililotokea New York, muda huo huo likafahamikia dunia nzima ndani ya muda mfupi.

Ajabu kabisa. Kwa watu wa imani hawashangai sana kwani tayari ilishatabiriwa kitambo.

Hata Mbora wa Viumbe, alishawahi kusema itafika zama dunia itakuwa kama kijiji, lakini wengi hawakumuelewa enzi hizo. Lakini kile kinachoonekana sasa, wengi wameelewa Mtume Muhammad (SAW) alikusudia nini.

Kutokana na dunia kuwa kijiji leo wengi tunakubaliana wasanii wa mataifa mengine wanatumia muda mrefu kuumiza kichwa kufikiria wafanye nini ili kazi zao zitoke zikiwa na ubora wa hali ya juu na kuteka mashabiki, wasanii wa Kibongo wanashindana kutafuta kiki ili kuchanganya watu.

Muangalie Harmorapa alivyowahi kuibuka na kiki alizofanya, kisha angalia kazi zake zilizopo hewani ndio utabaini ukweli ulivyo!

Achana na chipukizi huyo, fuatilia mastaa wengine wanapotaka kutoa kazi zao mpya na kiki wanazofanya, fuatilia stori za kimapenzi na picha zinazowekwa kwenye akaunti za wasanii hao ama kwenye mitandao mingine ya kijamii utaelewa nataka kulenga kitu gani.

Mara utasikia huyu sijui anatoka kimapenzi na demu yule, mara sijui Amber Lulu na Lulu Diva wana ugomvi wa kugombea jina, mbali na vituko vingine ambavyo havisaidii kuwafanya wawe wasanii wakubwa. Kila msanii hasa wa muziki wa kizazi kipya na wale wa filamu wanaamini katika kutengeneza kiki zaidi kuliko kupiga kazi.

Wengi wao wameshindwa kujifunza kwa Diamond ambaye baada ya kutembea kwenye kiki za kubadili wanawake kama nguo, aliamua kujikita kwenye muziki na sasa anapaa anga za kimataifa. Hawajifunzi kwa Alikiba, Lady Jaydee, Vanessa Mdee, Christian Bella na Gabo Zagamba na wengine wanaotisha katika fani zao ndani na nje ya nchi.

Juzi Ijumaa nikiwa naangalia kipindi flani katika chaneli moja ya DSTV niliona mahojiano ya wasanii wanaokuja juu kwa sasa wakieleza kuvunjika kwa ndoa yao. Sio hao tu, lakini kila uchao utasikia vituko vya wasanii na maisha yake binafsi kuliko kazi zao kisanii. Hii haivutii.

Suala la wasanii kuoana ama kuwa wapeznzi kisha kuachana na kuchafuana mitandaoni, wakati mwingine hufanyika kama fasheni ya kutaka kuwafanya mashabiki wawafuatilie kwa ukaribu.

Kwa sasa kuna baadhi ya mashabiki hawataamini tena stori zozote za mastaa kadhaa kwa sababu wanajua ni njia ya kutafuta kiki tu, yaani huko hawajambo kuliko kuzalisha kazi bora na zitakazowavusha anga za kimataifa. Wamebaki katika akili za enzi zile za bifu la kina Inspekta Haruna dhidi ya Sir Juma Nature ama TMK dhidi ya East Coast.

Hawajui tu wanavyowakera mashabiki wao ambao wanatamani kuona Diamond, Kiba, Lady Jaydee, Vanessa Mdee, Weusi ama Navy Kenzo wakipata wasanii wengine wa kuwaunga mkono kwenye kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa.

Ushauri wangu, wasanii wajikite kwenye kutengeneza kazi zitakazowatangaza nje ya nchi na kuwaingia mamilioni ya fedha na sio kubobea kwenye kusaka kiki, kiki nyingine zikiwadhalilisha wao na familia zao kiasi cha kutia aibu.

Mzazi gani anayefurahia kuona ama kusikia mwanae anabadili wanaume kama nguo, huku hata siku moja hajawahi kupokea angalau barua moja ya posa...Mzazi gani anayeweza kufurahia kuona kijana wake akifanya uchafu kwa kisingizio cha usanii? Kiki zinaweza kuwa na msaada wa muda, lakini zina udhalilishaji wa milele.

Tuachane na kiki hizo za wasanii, tuangalie soka ambalo kitaifa na kimataifa wikiendi hii kuna burudani zilizowapa raha na simanzi mashabiki wanaofuatilia mchezo huo.

Ukiachana na matokeo ya Simba na Azam ama yale ya jana ya Kombe la FA na hata katika Ligi Kuu mbalimbali za Ulaya, bado naamini mpaka sasa mashabiki wa soka wanaendelea kujiuliza kasi waliyokuja nayo KMC inayocheza Ligi Kuu kwa msimu wao wa kwanza.

Ukiangalia msimamo kwa sasa KMC ipo nafasi ya nne ikiwa na alama 40, baada ya kuanza msimu kwa kusuasua. KMC pia ilikuwa miongoni mwa timu zilizotinga 16 Bora ya Kombe la FA (ilitarajiwa kucheza jioni ya jana dhidi ya Mtibwa Sugar). KMC ni miongoni mwa timu zilizopoteza mechi chache baada ya Simba, Yanga na Azam, licha ya ugeni wao katika Ligi Kuu.

Inachokifanya KMC kwa sasa ni kama ilivyowahi kufanya Mbao FC katika msimu wake wa kwanza, ilivyokuwa ikishangaza mashabiki ikizitetemesha vigogo na hasa kuionea Yanga mara kadhaa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Kinachosisimua ni kwamba aliyeifanya Mbao iitishe Yanga na kuitetemesha Simba ni Etienne Ndayiragije ambaye kwa sasa ndiye anayeinoa KMC, ndio maana Vijana hao wa Kinondoni wanashangaza wengi kuanzia soka lao uwanjani mpaka matokeo inayoyapata katika Ligi Kuu.

Hakuna aliyekuwa akiidhania kama KMC ingetetemesha katika ligi kwa namna ilivyoianza ligi hiyo, huku ikiwa imewatema asimilia kubwa ya wachezaji walioipandisha na hata kocha wao, Fred Felix ‘Minziro’.

KMC ilishanza kama ilivyoshangaza Mbao pale ilipoajiri Kocha wa kigeni kutoka Burundi, Etienne Ndayiragije na kusajili nyota kadhaa wa kigeni wakiwamo wa kimataifa. Ilishangaza kwa sababu kuna baadhi ya timu zoefu za Ligi Kuu hazijawahi na wala hazijaota kufanya usajili kama huo. Usajili wa nyota wa kigeni umekuwa ni ligi ya klabu za Simba, Yanga na Azama na kidogo sasa Mbeya City au Stand United ilipokuwa na udhamini wa maana toka Kampuni ya Acacia kabla ya mkataba wao kuvunjika kwa sababu ya mgogoro.

Kama itaendelea na maajabu yake, haitashangaza kuona timu hiyo ikifika mbali, lakini cha kuwakumbusha mabosi wa klabu hiyo, moto walioanza nao msimu wao wa kwanza waendeleze hata msimu ujao.