NO AGENDA: SOMETIMES CHIDI BENZ ANARUDI VIZURI SOMETIMES DISH LINAYUMBA

Sunday February 24 2019

 

By Luqman Maloto

NAIHUSUDU ngoma “Ten Crack Commandments” ya Notorious BIG. Kwa Kiswahili chepesi, wimbo huo unaweza kuuita Amri 10 za Dawa za Kulevya.

Sababu ya kuipenda ngoma hiyo ni kuwa amri zote 10 kama ambavyo BIG a.k.a Big Small aliziorodhesha katika shairi lake kisha kuchana kwenye mdundo mzuri wa Hip Hop, zinajenga picha wauza unga ni watu wa namna gani.

BIG kwa kutambua wangeweza kutokea watu wakambishia katika hizo amri zake 10, anaanza kwa kutamba hakuna mtu wa kumwambia kitu kwenye biashara ya dawa za kulevya. Anasema aliifanya biashara hiyo kwa miaka kadhaa na ilimfanya awe mnyama.

Chukua mstari huo; biashara ya dawa za kulevya ilimfanya BIG awe mnyama. Maana yake ukiwa muuza dawa za kulevya unakuwa mnyama. Yaani unapoteza roho ya utu.

Amri zote nazikubali, lakini huvutiwa zaidi na amri ya nne; Never get high on your own supply.

Kiswahili: Kamwe usitumie unachouza.

Unapokuwa muuza unga unajua kuwa hicho ni kilevi cha maangamizi, kwa hiyo BIG anakufahamisha kuwa usijaribu kutumia, maana utaangamia.

Amri ya tano ni muhimu; never sell no crack where you rest at. I don’t care if they want a ounce, tell ‘em bounce!

Kiswahili: Usiuze dawa kwenye maeneo yako ya kujidai. Sijali kama watataka cha ukucha, waambie imegonga mwamba.

Ufafanuzi ni kuwa unga ni maangamizi, kwa hiyo unatakiwa kuuza mbali, siyo kwenye maeneo unayoishi, maana utawaangamiza watu wanaokuzunguka.

Ipo amri ya saba ambayo BIG anasema “tenganisha biashara na familia yako”, haitakiwi hata kidogo watu wa familia yako wahusike na uharamia wako ili ukipata msala ujikute matatizoni peke yako.

Amri ya nane pia anaelekeza “usijibebeshe mzigo mwenyewe”, ukiwa muuza unga unafahamu ni kimeo, kwa hiyo wabebeshe wengine ili wakikamatwa uwe msala wao.

UNAELEWA NINI?

Ten Crack Commandments imo kwenye albamu “Life After Death” ambayo ni ya pili na ya mwisho kwa BIG. Life After Death ilitoka Machi 25, 1997. Kipindi hicho Chidi alikuwa kinda tu pale Ilala Maghorofani.

Mantiki hapo ni kuwa Chidi alipopata maujanja na kukwea juu ya kilele cha Hip Hop ya Kiswahili, alikuta tayari forefathers wa Hip Hop duniani, walishachana sana kuhusu ubaya wa madude na namna yanavyoangamiza. Pamoja na hivyo, Chidi akayavagaa!

Namfahamu Chidi, ni mwana Hip Hop aliyekamilika. Sauti yake pekee ni mtaji. Anaweza kupanda, kushuka na kuigeuza alivyotaka, vilevile anayo staili inayomfanya awe wa kipekee. Ana swagger ambazo humpa mvuto anapotambaa kwenye mdundo wa boksi.

Chidi ana pumzi na nguvu akiwa jukwaani. Kwa tathmini yangu kama mwandishi wa habari, vilevile mdau katika soko la muziki na sekta ya burudani Tanzania kwa jumla, nathubutu kusema ndiye mwanamuziki wa Hip Hop Bongo ambaye hutumia nguvu nyingi jukwaani na kumudu kufanya shoo kwa muda mrefu tena kwa ufanisi.

Hujiuliza; kama huonesha uwezo huo jukwaani ilhali anatumia ‘madude’, je, angekuwa hatumii? Bila shaka angeweza kufanya zaidi. Jicho langu kimuziki linaniaminisha kuwa Chidi alizaliwa ili awe rapa.

Ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wa Hip Hop nchini wenye uwezo wa kutumbuiza kwa ‘live band’ na kukonga nyoyo za hadhira kwa kiwango cha juu. Kama wewe ni shabiki wa Hip Hop, unataka nini kingine pale Chidi anapokuwa jukwaani kifua wazi?

Muhimu zaidi ni kwamba Chidi ana nyota. Anapendwa sana, ndiyo maana pamoja na matatizo mengi ambayo amejisababishia, mashabiki bado wanamhitaji. Hawajawahi kumlaani wala kumsusa.

Chidi pamoja na utajiri wote huo alionao kwenye soko la muziki, amekuwa hawezi kujiokoa.

Madude yamekuwa yakimfanya apishane na mikwanja, wakati kuna kipindi alikuwa akitembea na mabulungutu ya fedha za BOT kwenye gari na msululu wa wapambe. Mashallah, Chidi alikula ujana!

KAMA KARUDI HIVI!

Juzikati kuna kipande cha video kilisambaa mno kwenye mitandao ya kijamii, kikimwonesha Chidi katika mahojiano na chombo kimoja cha habari. Katika video hiyo, Chidi anamshauri Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kujielekeza katika masuala ambayo yanahusu nafasi yake.

Chidi anasema Makonda amekuwa akijielekeza kwa wasanii ili wamsifie na kuacha mambo yenye kuhusu cheo chake. Anabainisha kuwa mwisho kabisa, wasanii huhitaji wapewe pesa.

Akishafeli kwa wasanii, watu watampima kwa yale atakayokuwa ameyafanya kama mkuu wa mkoa.

Akatolea mfano kushughulikia suala wafanyabiashara wa soko la Karume, upangaji wa vitu ili watu na magari yapite vizuri, akazungumzia kuhusu hali za vituo vya polisi na magereza, kwamba Makonda anatakiwa kwenda na kuangalia wanaowekwa mahabusu na wafungwa wanaishije na wanalala vipi?

Chidi alisema mazingira ya magereza yanatakiwa kuboreshwa kwa sababu hali ni mbaya. Alifafanua kuwa watu madarakani hujisahau, lakini yeye ameshalala mahabusu na waliokuwa mawaziri, kwa hiyo jela anaweza kwenda yeyote, akiwemo yeye Makonda au Rais John Magufuli akishatoka madarakani, ikiwa mambo hayatakuwa mazuri upande wake.

Ukisikiliza maneno aliyosema, utaona kwamba Chidi amenena kwa akili kubwa. Alichokizungumza kinapaswa kupewa uzito ndani ya mjengo wa Bunge. Ni sawa na kusema, Chidi alivaa thamani ya ubunge na kuzungumza mambo makubwa.

Hata hivyo, wakati mwingine Chidi bado dish linayumba. Mahojiano mengi anayofanya, amekuwa mwenye kujisifu ugomvi na kushusha lawama kwa ambao anadhani hawamjasaidia. Wakati mwingine anaonesha ana furaha, ila kipindi kingine anadhihirisha chuki za wazi. Chidi ni muongea hovyo!

Si Chidi yule ambaye alikongoroka na kubaki mfano wa Chidi tu, kwa sasa afya inarejea. Siyo yule wa kulala na udenda sababu ya alosto, Chidi wa sasa anajitambua. Zaidi siyo Chidi aliyetwambia anavaa madini ya kuungaunga. Wa sasa anapendeza.

Pamoja na hivyo, tukubali kuwa Chidi sometimes anakuwa fresh. Anavutia kumsikiliza.

Anatema madini kushinda baadhi ya wabunge mjengoni. Sometimes dish likiyumba Chidi anakuwa ovyo. Kila anachozungumza kinakuwa chengachenga tu. Bado anahitaji uangalizi akae sawa.