Thiago Alcantara akubali kutua Manchester United

Thursday September 13 2018

 

KIUNGO fundi wa mpira, Mhispaniola Thiago Alcantara amesema hatakuwa na kinyongo chochote katika kujiunga na Manchester United kama timu hiyo itakabidhiwa kwa Kocha Zinedine Zidane.

Staa huyo anayekipiga kwenye kikosi cha Bayern Munich kwa sasa alisema amesikia ripoti ya Zidane kuhusu wachezaji anaotaka kuwasajili kama atapewa kibarua cha kuinoa Man United kinachoshikiliwa na Jose Mourinho kwa sasa, hivyo yeye yupo tayari na anasubiri fursa hiyo kwa hamu.

Alcantara, ambaye mwaka 2013 aliwindwa sana na Man United wakati huo ilipokuwa chini ya David Moyes ni mmoja kati ya wachezaji waliopo kwenye orodha ya Zidane kama atatua Old Trafford kurithi mikoba ya Mourinho.

Mastaa wengine ambao Zidane anatamani kuwasajili atakapopewa kazi ya kuinoa Man United ni kiungo wa Real Madrid, Mjerumani Toni Kroos, kiungo wa Colombia, James Rodriguez na fowadi wa Paris Saint-Germain, Edinson Cavani.

Kibarua cha Mourinho kimeripotiwa kuwa kwenye hali mbaya huko Old Trafford licha ya makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Ed Woodward kuonekana kuweka mkazo bado anamwaamini kocha huyo Mreno.

Advertisement