Ten Hag kuonja machungu

Muktasari:

  • Ten Hag alisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuifundisha Man United mwaka 2022 na katika siku za hivi karibuni amekuwa kwenye presha ya kufukuzwa.

KWA mujibu wa ripoti kutoka ESPN, kocha wa Manchester United Erik Ten Hag atapoteza asilimia 25 ya mshahara wake ikiwa ataendelea kuifundisha timu hiyo kwa msimu ujao.

Ten Hag alisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuifundisha Man United mwaka 2022 na katika siku za hivi karibuni amekuwa kwenye presha ya kufukuzwa.

Kwa sasa mashetani wekundu wanashikilia nafasi ya sita baada ya kushinda mabao 4-2 dhidi ya Sheffield United juzi, ambapo kwa sasa wana utofauti wa alama 13 na Aston Villa iliyopo katika nafasi ya nne ya kufuzu Ligi ya Mabingwa.

Ripoti zinaeleza Ten Hag atatakiwa kukatwa asilimia 25 ya mshahara wake kwa mwaka ikiwa atashindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu Ligi ya Mabingwa.

Hiyo ina maana kwamba msimu ukimalizika bila ya kufuzu basi msimu ujao atakuwa anakunja Pauni 6.75 milioni lakini hakuna uhakika ikiwa ataendelea kuifundisha timu hiyo.

Matokeo ya hivi karibuni yameonekana kuwakera sana mashabiki wa timu hiyo ambao ripoti kutoka England zinaeleza kwamba wamesusa hadi kuhudhuria uwanjani.

Moja kati ya mambo yaliowakera sana ni kuingia fainali ya FA dhidi ya Coventry kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Mchezo huo uliopigwa katika dimba la Wembley ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Man United kama Avram na Joel Glazer sambamba na tajiri mpya Sir Jim Ratcliffe ambaye ndio anasimamia shughuli zote za mpira wa miguu. Ratcliffe pia alikuwa na mkurugenzi wa masuala ya ufundi Jason Wilcox na taarifa zinaeleza kwamba hata wao hawakupendezwa na aibu hiyo, hivyo lolote linaweza kutokea.

Makocha kibao kama Graham Potter na Roberto de Zerbi wamekuwa wakihusishwa kuwa katika mazungumzo ya kuchukua mikoba ya Ten Hag.