Tatizo sio Pogba wala si Mourinho

Sunday September 30 2018Badru Kimwaga_micharazomitupu@gmail.com

Badru Kimwaga_micharazomitupu@gmail.com 

By BADRU KIMWAGA

JANA Man United ilikuwa uwanja wa London kuvaana na wenyeji wao, West Ham United na kulala kwa mabao 3-1. Tuachane na matokeo ya mchezo huo, lakini tunajua kuna sarakasi zinaendelea baina ya Kocha Jose Mourinho na kiungo Paul Pogba.

Wawili hao wamekuwa hawana uhusiano mzuri. Mounrinho amekuwa akimkosoa waziwazi Pogba. Huku Pogba wakati mwingine akimuonyesha kiburi kocha huyo. Kama ilivyo siku zote, mafahari wawili huwa hawakai zizi moja. Mourinho ni fahari mmoja na Pogba fahari mwingine. Kilichopo baina yao ni kama ukoo wa kambale kila mmoja ana ndevu kiasi hujui nani mkuu.

Mzozo wao ulichochewa zaidi mwezi uliopita wakati Pogba alipodokeza anataka kuondoka OT ili akatafute maisha Camp Nou. Hili lilimkera Mourinho kabla ya mambo kutulia na kuja kuibuka tena hivi karibuni kwa sababu ya mkasa wa Instagramu.

Nyuma ya filamu hii ya Pogba dhidi ya Kocha wake kuna darekta anayoiongoza. Mtu mmoja mjanja mjanja anayejua kutafuta fedha. Mino Raiola ndiye injinia wa ishu nzima, japo Mourinho kushindwa kukaa vyema na wachezaji nako ni tatizo. Ndio, haiwezekani kocha timu ikifanya vibaya umshambulie wachezaji moja kwa moja.

Ni busara ndogo alizonazo Mreno huyo, ndiyo inayomfanya akiulizwa lolote kutokana na matokeo ya mechi hizo humtaja yeyote anayeamini amevurunda uwanjani. Sio kama Pep Guardiola ambaye timu yake ikipata matokeo mabaya ueleza kiufundi na kusisitiza wanaenda kujipanga kiwa mechi ya mbele yao.

Sio kwamba haumizwi na matokeo, lakini Pep anatumia busara ya kuwastiri wachezaji wake, kwani inawezekana kabisa wakiwa vyumba vya kubadilishia nguo huwasema na hata kumtaja aliyewazingua. Makocha wenye busara wanapaswa kufanya hivyo. Wachezaji ni watu wazima, wana familia na watu wanaoheshimiana nao. Wanaposhambuliawa hadharani, wakati mwingine hujenga kiburi.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba Raiola mkono unawasha. Anatamani kushika noti tena. Alivuna za kutosha alipomtoa Pogba kutoka Juventus kuja Old Trafford. Anajua wazi akichochea moto huu pale OT, ni rahisi Pogba akachomoka, iwe ni kurudi Juventus ama kwenda Barca, lakini muhimu kwake ni kuvuna kitita cha mgano wa mauzo ya nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa. Sio mara ya kwanza kufanya hivyo, ndivyo Mawakala wanaovuna fedha bila kutoka jasho wanavyojua kucheza kiakili.

Hata Mourinho alishashtuka na kumchana wazi kwamba anamharibia timu, baada ya kuanzisha chokochoko zake kwamba mteja wake hana furaha OT. Anajua Pogba atauzwa zaidi ya fedha zilizomrudisha Man United. Lakini pia, kwa hali ilivyo OT ni vigumu mafahari hao wawili kukaa zizi moja. Ni mawili ama Pogba aruhusiwe tu kuondoka OT ama asalie na mkono wa kwaheri apewe Mourinho.

Hata mashabiki wa Man United wanatamani hilo litokee, yaani mmoja aondoke, lakini turufu ikiwa wazi kwa Mourinho wakitaka asepe kikosini kuliko kumuona Pogba anaondoka na soka lake. Wanaamini ni aina ya wachezaji wenye vipaji, ila anashindwa kufanya yake mavituz kama yale ya Russia alipoisaidia Ufaransa kubeba tena taji la Dunia kwa kuigaragaza Croatia.

Hata hivyo wanasahau kuwa wanaweza kuwakosa wote kwa pamoja, Mourinho akafurushwa kwa soka lake lisilovutia wala mbinu za ushindi, huku Pogba naye akisepa kwa kuwa tu, Raiola anataka umatemate. Ndivyo anavyoendesha maisha yake kiujanja ujanja kupitia nyota kama hao anaowalimiki bila jasho.

Advertisement