Pogba ashusha silaha kali Man Utd

Thursday September 13 2018

 

MAISHA ndivyo yalivyo, safari moja huanzisha nyingine. Umesikia hii ishu ya usajili matata kabisa unaotajwa utafanyika kwenye dirisha la Januari? Manchester United na Juventus zinadaiwa zitafanya dili moja la kibabe.

Utashangaa kitakachotokea. Man United na Juventus zinapanga kuingia kwenye dili matata ambalo litawahusu Cristiano Ronaldo, Paul Pogba, Paulo Dybala na Douglas Costa.

Unaambiwa hivi, uhamisho wa Ronaldo kwenda Juventus, unashikilia huduma za masupastaa watatu. Pogba huko Man United na Dybala na Douglas Costa huko Juventus. Ni hivi, Dybala hajatulia tangu Ronaldo alipotua Juventus. Anachotaka ni kuondoka tu kwenye timu hiyo.

Kusikia hivyo tu, Man United imetangaza kumtaka. Lakini, Juve baada ya kumpata Ronaldo, inamhitaji pia Pogba kuifanya kuwa balaa zaidi uwanjani. Kusikia hivyo, Man United ikaja na ishu nyingine, itamhitaji Douglas Costa kuwa sehemu ya dili hilo.

Juventus imeambiwa kama inamtaka Pogba, basi itapaswa kuwaachia Dybala na Douglas Costa wakatue Man United. Hiyo ndiyo biashara ya kubadilishana wachezaji inayotarajiwa kufanywa kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji Januari.

Hata hivyo, mpango huo unaweza kuharibika kama Barcelona itatumia nguvu ya pesa kumsajili Pogba. Lakini, Man United haiwezi kukubali kufanya biashara isiyokuwa na faida kwani, inaamini Pogba akienda Juventus, basi itakuwa na nafasi nzuri ya kuwachukua wachezaji wawili wa maana, Dybala na Douglas Costa, ambao wakitua Old Trafford, mastaa hao wa kutoka Amerika Kusini wataifanya Man United kuwa matata zaidi uwanjani.

Timu hizo zote mbili, Juventus na Man United zimelenga kufanya biashara itakayokuwa na maana katika kuboresha makali ya vikosi vyao na kufanya vyema kwenye ligi za ndani na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Advertisement