Pogba aaga Old Trafford, United wagoma

KAZI ipo. Bundi bado anaunguruma Old Trafford. Wakati Kocha Jose Mourinho akilalamika klabu kutonunua wachezaji, ndio kwanza mastaa wake wengine wanataka kuondoka klabuni hapo na kuleta utata zaidi.

Paul Pogba amewaambia wachezaji wenzake pamoja na wafanyakazi wa klabu hiyo anataka kuondoka klabuni hapo na kutimkia Barcelona kabla ya kufungwa kwa dirisha hili la uhamisho wachezaji kesho usiku.

Kama vile haitoshi, Pogba ambaye ni staa wa kimataifa wa Ufaransa amemtumia ujumbe wa simu ya mkononi Bosi Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward akimweleza nia yake ya kuondoka klabuni hapo ingawa inaeleweka United ilikataa hapo hapo.

United imeendelea kusisitiza staa huyo hauzwi ikiwa ni siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho huku kesho ikitarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya msimu dhidi ya Leicester City.

Mabosi wa United wanaamini watakuwa na nafasi ndogo ya kupata mbadala wake kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo na wamemshutumu wakala wake, Mino Raiola kwa kushinikiza uhamisho wa staa huyo kwenda Barcelona kutokana na tamaa zake za pesa.

Sasa kuna uwezekano mkubwa wakakumbana na jinamizi la kumbakisha mchezaji asiye na furaha klabuni hapo huku akiwa anaingiza mshahara wa Pauni 9.62 milioni kwa msimu ukijumlisha na kiasi cha Pauni 3.78 milioni kama bonasi.

Inaaminika Pogba amekubaliana maslahi binafsi na Barcelona na atachukua mshahara wenye thamani ya Pauni 89.5 milioni kwa miaka mitano ikiwa ni mshahara wa Pauni 18 milioni ambazo ni sawa na Pauni 346,000 kwa wiki.

Inaeleweka Pogba anataka kucheza Hispania na staa wa Argentina, Lionel Messi pamoja na staa mwenzake wa zamani wa Juventus, Arturo Vidal, ambaye alijiunga na Barcelona wiki iliyopita akitokea Bayern Munich.

Pogba amechoshwa na maisha ya United chini ya Kocha Mourinho ambaye amekuwa akimshambulia mara kwa mara hadharani na aliudhika zaidi baada ya kocha huyo Mreno kushindwa kumsifu kwa mafanikio yake aliyopata Russia na kikosi cha Timu ya Taifa ya Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia.

Badala yake Mourinho aliamua kuhoji kuhusu kujituma kwa Pogba katika kikosi cha Ufaransa pamoja na tabia zake kwa jumla.

Tabia hiyo ya Mourinho ilianza tangu msimu uliopita na alimweka nje katika baadhi ya mechi muhimu.

Kwa sasa mambo yamebadilika zaidi baada ya Pogba kurudi katika kambi ya mazoezi ya United, Carrington akitokea likizo Marekani na anataka kuondoka katika klabu hiyo ambayo ilivunja rekodi ya uhamisho miaka miwii iliyopita kwa ajili ya kumnasa.

Inaaminika tangu Aprili mwaka huu, Mourinho alikuwa tayari kumuuza Pogba katika dirisha hili la majira ya joto lakini itakuwa ngumu kumuuza kwa siku ya leo kutokana na kutojiandaa kupata mbadala wake.

Tayari inadaiwa United imekataa ofa ya awali ya Barcelona ambayo ilitaka kuipa Manchester United kiasi cha Pauni 44 milioni pamoja na mastaa wawili, Andre Gomes na beki Yerry Mina ambaye imekuwa ikimfukuzia katika siku za karibuni.

Hata hivyo, Mina ambaye ni staa wa kimataifa wa Colombia inasemekana anaenda Everton baada ya klabu hiyo ya England kukubaliana dau la Pauni 28 milioni kwa staa huyo aliyetamba katika Kombe la Dunia.

United imepokea habari mbaya baada ya beki wa kimataifa wa Ujerumani wa Bayern Munich, Jerome Boateng kudaiwa kumpigia simu Mourinho na kumwambia hana mpango wa kukipiga Old Trafford licha ya kumshukuru kwa kumwamini na kutaka kumchukua.