Pesa lazima iongee!

Friday May 17 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

ED Woodward jina gumu sana kujiita kwa kipindi hiki. Kwa sababu Manchester United wote duniani, kuanzia wachezaji, makocha na hata mashabiki, wote wanamkodolea macho yeye.

Wanamtazama waone atakachokifanya kwenye dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi kuinusuru timu hiyo. Ed Woodward ndiye makamu mwenyekiti wa Man United - ndiye anayehusika na mambo ya usajili, hivyo shughuli pevu inamkabili.

Man United isipopata wachezaji inaotaka kusajili, lawama zote kwake, hana pa kujificha. Ndiyo maana ngumu kuwa Ed Woodward kwa kipindi hiki. Anasukumwa na benchi la ufundi. Anasukumwa na mashabiki na anasukumwa na wamiliki wa timu. Presha kila kona.

Woodward kwa sasa yupo kwenye presha kutoka kwa wamiliki kisa Man United imeshindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Timu hiyo haitakuwapo kwenye michuano ya Ulaya na imeachwa pointi 32 na Manchester City kwenye Ligi Kuu England. Woodward tayari ameshabadili makocha mara nne ndani ya muda mfupi na kuitia timu hasara. Hivyo anahitaji kuwa na utulivu kwenye dirisha hili la usajili kupata mastaa watakaobadili hali huko Old Trafford. Man United imepoteza makali yake tangu iwe chini yake. Tofauti na ilivyokuwa kwenye enzi za David Gill.

Woodward ametumia pesa nyingi kusajili, pesa nyingi kulipa mishahara, lakini kikosi kinachoshindwa kushindania ubingwa na Man City na Liverpool.

Advertisement

Sawa, Woodward anatumia anachokiingiza. Akiwa bosi, Man United imepata mapato ya Pauni 590 milioni. Amesaidia kuifanya Man United kuendelea kutamba kwenye chati za klabu tajiri duniani.

Lakini anafeli kwenye usajili. Makocha watatu David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wote wamekuja na kuondoka kwa kulipwa pesa nyingi za fidia. Anaelekea kwenye kumlipa fidia pia Ole Gunnar Solskjaer kama hatafanya usajili makini kwenye dirisha lijalo. Paul Pogba amemnasa kwa Pauni 89 milioni, Romelu Lukaku kwa Pauni 75 milioni na anamlipa Alexis Sanchez mshahara wa Pauni 505,000 kwa wiki, wote hasara kubwa. Mourinho alisema hivi karibuni Man United bado inafanya mambo yake kizamani.

Jambo hilo linawasumbua kwenye kupata wachezaji makini, ambao bila shaka watahitaji kwenda kucheza Juventus, Real Madrid, Barcelona na Paris Saint-Germain kwenye uhakika wa kucheza michuano ya Ulaya.

Huo ni mtihani mwingine kwa Woodward kunasa wachezaji mahiri waje kucheza kwenye timu ambayo kwa msimu ujao haitakuwapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Atawashawishi vipi? Ni kutumia pesa tu.

Zaidi ya hilo basi ni kwenda kuhangaikia usajili wa wachezaji kama Bruno Fernandes, Gelson Fernandes na Idrissa Gueye. Ndiyo aina ya wachezaji wanaotajwa kuhusishwa na Manchester United kwa sasa baada ya kushindwa kuwapo kwenye Top Four. Hakuna tena kuwasajili mastaa kama Neymar, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe, Philippe Coutinho, Toni Kroos, Gareth Bale na mastaa wa aina hiyo wa kiwango cha dunia.

Waje Old Trafford kufanya nini au kucheza michuano gani, Europa League? Mastaa kama hao wataweza kutua Old Trafford kwa kutumia mvuto wa pesa tu, pesa lazima iongee!

Advertisement