Breaking News
 

Mo Salah? Wee Liverpool watabisha tu

Friday January 12 2018

 

LIVERPOOL, ENGLAND

HII kitu usiwaambie kabisa mashabiki wa Liverpool hawawezi kukuelewa. Kwamba eti, inasemakana Mohamed Salah ndiye mchezaji aliyepoteza nafasi nyingi za wazi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Salah huyu huyu. Huyu huyu unayemfahamu, mwenye mabao 17 kwenye Ligi Kuu England hadi sasa na anayevutia kumtazama mpira unapokuwa kwenye miguu yake huku akifukuzia kimyakimya Kiatu cha Dhahabu.

Lakini, kwa data zilizokusanywa na Arseblog, zinaonyesha kwamba Salah anaongoza kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi zilizokaribia kuwa mabao baada ya kufanya hivyo mara 15 na kufuatiwa na straika wa Chelsea, Alvaro Morata, aliyekosa nafasi 14.

Mastaa wa Man City, Sergio Aguero na Gabriel Jesus wanashika nafasi ya tatu na nne kwa kukosa nafasi 12 na 11 mtawalia, huku Christian Benteke wa Palace akikamilisha tano bora akikosa nafasi 11. Kwa namna ambavyo Salah amekuwa akitupia msimu huu ni jambo gumu kukubali kwamba anaongoza kwenye kupoteza nafasi, lakini ukweli unabaki palepale kuwa kama angetumia vizuri nafasi zote alizopata, angeshatupia mabao 30 huko.