Huyo Mbappe balaa tupu

Tuesday May 21 2019

 

PARIS, UFARANSA

MPO? Huyu Kylian Mbappe sio mtu mzuri, anataka kusababisha Vita ya Tatu ya Dunia. Unajua kwanini? Juzi Jumapili wakati akipokea tuzo yake ya kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka huko Ufaransa, akasema ameshamaliza kazi yake PSG na sasa anafikiria kwenda kukabiliana na changamoto mpya kwingineko.

Kwa lugha nyepesi fowadi huyo wa Ufaransa aliyebeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 akiwa na kikosi cha Les Blues anajiandaa kuachana na timu yake hiyo ya PSG, amejiweka sokoni.

Mbappe alisema huu ni wakati wake wa kwenda kupambana na changamoto mpya, akisema: “Hili ndiyo taji pekee nililokuwa nalisaka, sasa nimefurahi. Nimesema nilichopaswa kusema. Unapokuwa kwenye nafasi ya kutuma ujumbe, basi tuma huo ujumbe, nimeshatuma wa kwangu. Kama nikiongea itakuwa maneno mengi na hapo ujumbe wangu utakuwa haujafika.”

Kitendo cha Mbappe kudai yupo tayari kuondoka kitaziingiza kwenye vita kali klabu vigogo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitamani kuwa na huduma ya mchezaji huyo.

Real Madrid, Manchester City, Barcelona, Arsenal, Manchester United, Juventus, Chelsea na hata Bayern Munich bila ya shaka zitakuwa kwenye vita kali ya kufukuzia saini yake. Real Madrid inataka kujijenga upya, hivyo bila ya shaka Kocha Zinedine Zidane anafukuzia fursa ya kuwa na huduma ya Mbappe, ambapo awali ilidaiwa kwamba imetenga Pauni 246 milioni kwa ajili ya kumnasa. Lakini Barcelona nayo inatafuta mrithi wa Luis Suarez jambo litakalomfanya Kocha Ernesto Valverde kupambana kuinasa saini yake, huku Man United, Kocha Ole Gunnar Solskjaer anaweza kuchangamka kumnasa mchezaji huyo ambaye pia atakuja kutumika kama nembo ya klabu kwenye mambo ya kibiashara kama Paul Pogba atatimkia zake Bernabeu.

Advertisement

Pep Guardiola wa Man City anaweza kutaka huduma ya mshambuliaji huyo ili kumbadili Sergio Aguero, ambaye umri unaanza kumtupa mkono huku Chelsea ya Maurizio Sarri inaweza kumsajili kama itafutiwa adhabu ili kwenda kuwaondoa katika presha Eden Hazard akiondoka.

Liverpool pia inaweza kuwa na nafasi nzuri ya kumbeba Mbappe ili kumfanya Kocha Jurgen Klopp kutengeneza kikosi imara sawa na ilivyo kwa Mauricio Pochettino huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur.

Arsenal kuna wakati ilipokuwa chini ya Arsene Wenger ilijaribu kumnasa fowadi huyo, lakini sasa inaweza kupata urahisi chini ya Unai Emery kwa sababu alikuwa naye kwenye kikosi cha PSG kinachovaa jezi za Emirates kabla hajaenda Emirates Stadium. Kwa kifupi tu, vikosi hivyo sambamba na Juventus na Bayern ndivyo vyenye uwezo wa kumnasa.

Changamoto kwa Arsenal ipo kwenye bajeti yake ya usajili. Mbappe ametua PSG kwa ada ya Pauni 166 milioni na katika misimu yake miwili aliyoitumikia timu hiyo amefunga mabao 45 kwenye mechi 55 za Ligue 1 na kumfunika kabisa Neymar. Mkataba wake unafika tamati 2023, hivyo bei yake haishikiki.

Advertisement