Hazard anauzwa Pauni 225 milioni

Tuesday August 7 2018

 

NDIO kama mlivyosikia. Chelsea iliweka ngumu kabisa kumwachia staa wake, Eden Hazard ambaye anasakwa kila kona na Real Madrid, lakini sasa kila kitu kiko wazi.

Real Madrid imeambiwa kama inaitaka saini ya Hazard basi ijiandae kuweka mezani Pauni 225 milioni ambalo ni dau la rekodi mpya ya dunia.

Kwa sasa rekodi ya usajili wa pesa nyingi inashikiliwa na Neymar, ambaye alinaswa na PSG akitokea Barcelona kwa Pauni 198 milioni.

Kwa muda mrefu sasa Hazard alikuwa akitajwa kuwa mrithi sahihi ya viatu vya Mreno, Cristiano Ronaldo ambaye tayari ameondoka zake na kutua Juventus kwa dau la Euro 112 milioni.

Kuondoka kwa Ronaldo ni Dhahiri, mabosi wa Real Madrid wataongeza nguvu kwa Hazard kuhakikisha anapeleka makali yake na kuifanya kuwa tishio na Rais wa Los Blancos, Florentino Perez anataka kurejesha heshima ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbali na Hazard, Madrid pia imekuwa ikihusishwa na usajili wa mastaa wengine kama Harry Kane (Spurs), Robert Lewandowski (Bayern Munich), Neymar na Kylian Mbappe wote wa PSG ambao kwa sasa hakuna dalili ya kuwanasa.

Lakini taarifa za ndani kutoka Chelsea zilizoripotiwa, zimeeleza Hazard anaweza kuondoka kama tu Madrid italipa ada ya Pauni 225 milioni.

Kwa upande wa Hazard mwenye umri wa miaka 27, mara kadhaa ameweka bayana kuwa ndoto yake ni kuichezea Real Madrid na mpaka sasa ameshindwa kuweka wazi kama atabaki Chelsea ama ataondoka kujiunga na timu hiyo.