HE! Pogba kampigia simu Sarri huko

MANCHESTER, ENGLAND,

UTASIKIA mengi kwenye kipindi hiki cha usajili. Kinachosemwa kwa sasa ni kiungo Paul Pogba amempigia simu Kocha Maurizio Sarri akimtaka afanye kweli kumsajili ili aachane na Manchester United dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Supastaa huyo wa Ufaransa, amelenga kuachana na maisha ya Old Trafford dirisha hili na hivyo kuamua kufanya uamuzi wake mwenyewe kuhakikisha anaondoka.

Kwa mujibu wa According to Tuttosport, Pogba amempigia simu kocha huyo mpya wa Juventus akijaribu kumshawishi amsajili. Ripoti zaidi zinadai anachotaka Pogba kwa sasa ni kurudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani ya huko Italia.

Hivi karibuni akiwa huko Asia katika ziara yake ya mambo ya promosheni, Pogba alikiri kwamba amejiandaa na changamoto mpya kwingineko.

Man United yenyewe ilimrudisha kwenye kikosi chao mwaka 2016 baada ya kumnasa kwa pesa nyingi, Pauni 89 milioni kutoka Juventus.

Lakini, miaka mitatu baada ya uhamisho huo, Pogba sasa anataka kuhama Old Trafford huku mpango wake ni kurudi Turin. Real Madrid nao wamekuwa wakitajwa kuwa na mpango wa kumsajili staa huyo wa Les Bleus.

Kocha Sarri amerudi Italia kujiunga na Juventus ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kujiunga na Chelsea. Huko Juventus amesaini mkataba wa miaka mitatu.

Juventus wanakaribia kumnasa kiungo Adrien Rabiot kwa uhamisho wa bure baada ya mkataba wake kufika mwisho huko Paris Saint-Germain.

Kuhusu Pogba, Man United wameweka dau la Pauni 150 milioni kwenye kichwa cha mchezaji, anayemtaka basi aweke mzigo mezani.

Mkurugenzi wa michezo wa Juventus, Fabio Paratici amesema wanamtaka Pogba na kusema akimzungumzia staa huyo na Rabiot,

“Ni wachezaji wazuri. Lakini, Pogba ni mchezaji wa Manchester United. Alitufanyia mengi, alikulia hapa, tunampenda. Lakini ni mchezaji wa Man United. Kuhusu Rabiot kuna timu nyingi zinamtaka, tutafanya juhudi zetu, tutazungumza na Sarri kuhusu yeye.”