Bayern yamgeukia Rashford

Muktasari:
- Rashford amekuwa akihusishwa na Barcelona ambayo ameweka wazi kuwa ni ndoto yake na angetamani ajiunge nayo katika dirisha hili.
BAYERN Munich imeingia katika harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 27, baada ya kuvutiwa na kiwango chake alichoonyesha akiwa na Aston Villa kwa mkopo msimu uliopita.
Rashford amekuwa akihusishwa na Barcelona ambayo ameweka wazi kuwa ni ndoto yake na angetamani ajiunge nayo katika dirisha hili.
Mara kadhaa ripoti pia zilieleza kwamba amekuwa akizungumza na kinda wa wababe hao, Lamine Yamal ambaye ndio amependekeza pia kwa kocha Hansi Flick amsajili.
Mkataba wa Rashford unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na yupo katika orodha ya wachezaji ambao Man United inahitaji kuwauza katika dirisha hili kwani hayupo kwenye mipango ya kocha Ruben Amorim.
Rashford ambaye nusu ya msimu uliopita aliimalizia katika kikosi cha Villa alikokuwa akicheza kwa mkopo, ni miongoni mwa wachezaji wanaokunja pesa nyingi katika Ligi Kuu England ambapo mshahara wake kwa wiki ni pauni 300,000.
Ousmane Diomande
CRYSTAL Palace imefikia makubaliano ya kulipa pauni 47 milioni kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ivory Coast, Ousmane Diomande, mwenye umri wa miaka 21, kutoka Sporting Lisbon.
Beki huyu anatazamwa kama mbadala wa beki wa England mwenye umri wa miaka 24, Marc Guehi anayetarajiwa kuondoka katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi.
Davide Frattesi
MANCHESTER United imewasiliana na Inter Milan kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa timu hiyo na Italia, Davide Frattesi, mwenye umri wa miaka 25.
Frattesi amelivutia benchi la ufundi la Man United kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu msimu uliopita ambapo alicheza mechi 47 za michuano yote.
Noni Madueke
ARSENAL tayari imewasilisha ofa nono kwenda kwa winga wa Chelsea na England, Noni Madueke, mwenye umri wa miaka 23, ambaye ameomba kuondoka katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Madueke ambaye pia kiwango chake kinadaiwa kuwa hakimvutii sana kocha Enzo Maresca, anatamani kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Jhon Duran
MSHAMBULIAJI wa Al Nassr na timu ya taifa ya Colombia, Jhon Duran, mwenye umri wa miaka 22, amesafiri kwenda Uturuki kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wa mkopo kutoka Al-Nassr kwenda Fenerbahce. Inaelezwa staa huyu aliomba kurudi tena barani Ulaya kwa ajili ya kucheza soka la kiushindani ikiwa ni msimu mmoja tu tangu ajiunge na Al Nassr ya Saudi Arabia.
Leonardo Balerdi
NEWCASTLE inachunguza uwezekano wa kumsajili beki wa kati wa Marseille na timu ya taifa ya Argentina Leonardo Balerdi, mwenye umri wa miaka 26, ambaye pia anawindwa na Juventus.
Balerdi ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Marseille na msimu uliopita alicheza mechi 29 za michuano yote.
Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Tolu Arokodare
BURNLEY inatafuta shambuliaji mpya kwa ajili na staa wa KRC Genk na timu ya taifa ya Nigeria, Tolu Arokodare, mwenye umri wa miaka 24, ni miongoni mwa wale inaowahitaji.
Arokodare ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Genk na msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 23.
Jonathan David
JUVENTUS iko karibu kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa zamani wa Lille na timu ya taifa ya Canada, Jonathan David, mwenye umri wa miaka 25, ambaye mkataba wake na Lille uliisha mwisho wa msimu uliopita.
Kabla ya kufikia makubaliano na Juventus, mshambuliaji huyu pia alitajwa kuwa huenda angetua England.