Chama la wababe watupu uwanjani

Muktasari:

  • Hata hivyo, wachezaji wakorofi na wacheza rafu uwanjani si yeye tu, wapo kibao kiasi ambacho wanaweza kuunda kikosi chao cha kwanza chenye uwezo wa kushinda mechi na pengine hata ubingwa.

KWENYE soka kuna wachezaji hao wamekuwa kipenzi cha mashabiki wa timu pinzani kwa ajili ya kuwazoea tu kutokana na rafu zao wanazocheza uwanjani. Sergio Ramos ni mmoja wao na ndio maana mapema tu alisema anaamini Waingereza hawatamzomea kwa sababu rafu aliyomchezea Mohamed Salah haikuwa ya makusudi.

Hata hivyo, wachezaji wakorofi na wacheza rafu uwanjani si yeye tu, wapo kibao kiasi ambacho wanaweza kuunda kikosi chao cha kwanza chenye uwezo wa kushinda mechi na pengine hata ubingwa.

Hiki hapa kikosi cha wachezaji wakorofi uwanjani, ambao ukikutana nao, basi ujiandae, maana wenyewe ni ngumi mkononi.

Anthony

Lopes, kipa

Kipa wa Lyon, Anthony Lopes ni mmoja wa wachezaji wachafu sana uwanjanni.

Hajawahi kuwa na hofu ya kuwachezea rafu wachezaji wa timu pinzani bila ya kujali madhara gani yatatokea.

Mwishoni mwa msimu uliopita, alifungiwa mechi tano baada ya kugombana na mlinzi wa uwanjani huko Marseille. Ni kipa mkorofi kweli kweli anapokuwa ndani ya uwanja.

Sergio Ramos, beki wa kulia

Sergio Ramos amekuwa mtu anayechukiwa sana na hii ni kutokana na uchezaji wake wa ndani ya uwanja. Anacheza kibabe sana na rafu yake kwa Mohamed Salah iliyomsababishia matatizo makubwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, basi imemfanya awe adui mkubwa wa watu. Lionel Messi anamfahamu vyema beki huyo kwa jinsi ambavyo amekuwa akimchezea pindi timu zao zinapomenyana kwenye El Clasico.

Patrice Evra, beki wa kushoto

Kuna mambo mengi hakika unayoweza kumwelezea Patrice Evra, lakini yote kwa yote, beki huyo wa kushoto anafahamu aina zote za mchezo, ukitaka rafu twende, ukitaka kucheza kistaarabu basi sawa. Lakini, Evra hajawahi kuwa mstaarabu kwa mshambuliaji ambaye anasumbuasumbua. Kuna shabiki mmoja aliona jinsi akili ya mchezaji huyo ilivyo wakati alipomletea mambo ya kijinga, alimfuata na kumrukia daruga hakujali kama ni shabiki wa timu yake au la. Akaondolewa huko Ufaransa.

Pepe,

beki wa kati

Pepe amekuwa akiwatisha sana washambuliaji wa timu pinzani kiasi cha kuwafanya wakati mwingine kuumpa tu mpira wenyewe. Anapoona mshambuliaji amekuwa msumbufu ndani ya uwanja, basi ni lazima atachezewa kibabe sana na rafu atapigwa za kutosha tu. Mwaka 2009, Pepe alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu kiungo wa Getafe, Javier Casquero ndani ya boksi na kumpiga mateke baada ya kumwaangusha.

Alimkandamiza uso kwenye nyasi na alifanya hivyo mara nyingi kwa kadri alivyotaka. Pepe hajawahi kuwa beki mwepesi uwanjani.

Giorgio Chiellini, beki wa kati

Chiellini pengine anaonekana ni mmoja wa mabeki bora kabisa wa kati duniani. Lakini, ukweli usiofichika, ni mchezaji anayecheza soka la kibabe sana kwa wachezaji wenzake. Anapokuja kukukaba, basi tegemea tu Chiellini atakusukuma, kukugongagonga na kucheza rafu zile mbaya zinazoomiza. Mipango yake siku zote ipo katika kuhakikisha washambuliaji wa timu pinzani wanapata majeraha ambayo yatawafanya washindwe kufurahia mchezo.

Felipe Melo,

kiungo wa kati

Wenzake walimpachika jina la “The Pitbull” au “Gladiator”. Kupembana na kiungo Felipe Melo basi ilipaswa ujipange kweli kweli. Melo amekuwa mchezaji maarufu kutokana na kucheza soka kibabe na jambo hilo limemfanya awe na marafiki wachache pia.

Kwenye kikosi cha Inter Milan alitengeneza pacha kwenye sehemu ya kiungo na mwenzake Gary Medel, basi hakika ilikuwa kazi ngumu kweli kweli kwa wachezaji wa upinzani, maana unapokutana nao ilikuwa imekutana na wanyama dimbani.

Gary Medel, kiungo wa kati

Ile paap, umekutana na Gary Medel basi utadhani ni yule Gattuso wa zama zile za AC Milan. Maumbo yao yanafanana na shughuli yao uwanjani, ule ubabe wao pia unafanana. Medel amekuwa akicheza soka la kibabe sana, hana hofu ya kuwaumiza wenzake jambo linalomfanya wachezaji wanaochuana naye uwanjani kucheza kwa tahadhali kubwa. Pengine hicho ndizo anachokitaka kiungo huyo wa kimataifa wa Chile, kuogopwa ndani ya uwanja ili aweze kutawala kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja.

Nigel De Jong,

kiungo wa kulia

Mdachi, De Jong alikuwa matata kweli kweli uwanjani. Ni aina ya mchezaji ambaye hana hofu ya kumrukia mpinzani wake mguu wa shingo kwenye mchezo. Kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2010 alionyesha ubabe wake wakati alipomrukia mguu wa mbavu kwa staili ya teke la ‘Kung Fu’ kiungo wa Hispania, Xabi Alonso ilitosha kuonyesha aina ya uchezaji wa De Jong ulivyo. Ni mchezaji ambaye siku zote hana hofu ndani ya uwanja na jambo hilo limewapa shida sana wachezaji wenzake ndani ya uwanja na kuibua hofu.

Arturo Vidal, kiungo wa kushoto

Akili ya kiungo Arturo Vidal anaijua tu mwenyewe. Kuhusu uchezaji tu, Vidal ni miongoni mwa wachezaji wachache sana kwenye mchezo huo wa soka hapa duniani ambao wanajaribu kucheza kwa kujituma katika kila mechi. Lakini, shida ni uchezaji wake, si mtu anayeona hasara kucheza rafu hata kama anadhani itakuwa na madhara kwa mchezaji mwenzake, yeye kitu cha msingi anachowaza kwa wakati huo ni kuhakikisha timu yake inapata matokeo mazuri. Jambo hilo limemfanya wachezaji wengi anaocheza nao kumhofia.

Diego Costa, mshambuliaji

Straika Diego Costa alionyesha watu yeye ni mtu wa aina gani kwenye Ligi Kuu England siku ambayo alitaka kumchapa Steven Gerard. Lakini, hilo halikuwa tukio pekee lenye utata lililowahi kufanywa na mshambuliaji huyo. Alishawahi kutibuana na kocha Antonio Conte pia na hicho ndicho chanzo cha kuondoka Chelsea. Ameshawahi kugombana na wachezaji wenzake ikiwamo Mbrazili Oscar, mtu mkimya sana wakati walipokuwa pamoja kwenye kikosi cha Chelsea.

Costa ameshawahi kuadhibiwa na FA kwa kitendo cha kumkanyaga makusudi kiungo wa zamani wa Liverpool, Emre Can kwenye nusu gainali ya Kombe la Ligi.

Luis Suarez,

mshambuliaji

Katika maisha yake yote ya soka, straika Luis Suarez amekuwa mtu wa matukio tu ndani ya uwanja. Matukio yake yote ni ya hatari, kutoka kumfanyia ubaguzi wa rangi yake Patrice Evra hadi kung’ata meno wachezaji wenzake mara tatu tofauti. Amekuwa na matukio mengine ya kupiga wenzake mateke na ngumi.Kwenye soka lake, amewahi kukosa jumla ya mechi 45 kutokana na matukio yake ya ovyo ovyo ndani ya uwanja ikiwamo la kuamua kudaka mpira makusudi uliokuwa ukitinga wavuni kwenye fainali za Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Ghana huko Afrika Kusini.