Sarri presha kibao Chelsea

Muktasari:

  • Kocha Maurizio Sarri ameanza kutia shaka huenda kikosi chake cha Chelsea kikashindwa kuonyesha upinzani kwenye ligi kuu England msimu huu na hata nafasi ya kuwapo kwenye Top Four ikakosekana.

LONDON, ENGLAND. KOCHA Maurizio Sarri ameanza kutia shaka huenda kikosi chake cha Chelsea kikashindwa kuonyesha upinzani katika kupigania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Kocha huyo Mtaliano amefika mbali akisema hata nafasi ya kuwapo kwenye Top Four ina mashaka makubwa pia.

Sarri aliwataka wachezaji kujiweka sawa kiakili ili kutengeneza mazingira ya kufikia mafanikio makubwa kwenye ligi msimu huu.

Kocha Sarri ametokwa na maneno hayo baada ya timu yake kuchapwa mara mbili katika siku za karibuni, ikianza na kipigo kutoka kwa Tottenham Hotspur Jumamosi iliyopita kabla ya Jumatano ya juzi Jumatano kukung’utwa 2-1 na Wolves huko Molineux.

Sarri anachofikiria kwa sasa ni kufanya kikao cha kukutana na wachezaji wake mmoja mmoja baada ya kuona jinsi wanavyopoteza mechi kijinga kwenye mchakamchaka huo wa Ligi Kuu England.

“Nadhani tulicheza vizuri kwa dakika 55 tu,” alisema Sarri.

“Tumefunga bao la kwanza, kisha ikawa 1-1, na hakika ilikuwa bahati mbaya kwa sababu ukweli tulikuwa tumeutawala mchezo.

Lakini ghafla tukawa timu tofauti kabisa tukaanza kucheza hovyo na sijui ni kwa sababu gani hata mimi sifahamu.

“Nina wasiwasi sana, sio kwa haya matokeo bali kwa namba, tulishindwa kuchukua tahadhali baada ya bao la kwanza. Hatukuonekana kuchukua tahadhali na hakika hilo ndilo linalonitia mashaka.”