Pogba yupo zake Macca kupiga dua

Friday May 17 2019

 

LONDON, ENGLAND

KIUNGO Paul Pogba ameamua kusahau yaliyotokea Manchester United na kuamua kwenda zake Macca katika kipindi hiki akiwa kwenye swaumu ya mfungo wa mwezi Ramadhan.

Staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa baada ya kumaliza tu majukumu yake ya kuitumikia Man United kwenye Ligi Kuu England na timu kumaliza msimu kwenye nafasi ya sita ameamua kwenda zake Macca ikiwa ni sehemu yake ya ibada katika kipindi hiki akiwa kwenye mfungo.

Staa huyo ameungana na beki wa Chelsea, Kurt Zouma, ambaye pia ni Muislamu.

Pogba alituma picha yake kwenye mtandao wa kijamii akiwa huko Saudi Arabia na kuandika: “Kamwe usisahau vitu muhimu katika maisha.”

Pogba huko nyuma aliwahi kwenda Macca kuhiji, ibada ambayo kila Muislamu mtu mzima amekuwa akitamani kuifanya katika kipindi cha uhai wake.

Advertisement

Staa huyo ameamua kutumia mwisho wake wa msimu huu kufanya ibada kuliko kuchukua ndege na kwenda kwenye viwanja vya starehe za wachezaji kama vile Las Vegas na Ibiza.

Anatarajiwa kuwapo kwenye kikosi cha Ufaransa kitakachocheza mechi za kuwania kufuzu Euro 2020 mwezi ujao kabla ya kuamua hatima yake kwenye soka lake la klabu ambapo Real Madrid chini ya Kocha Zinedine Zidane imedaiwa kufukuzia saini ya mchezaji huyo.

Ripoti zinadai mshahara ni kitu kinachoweza kuzuia uhamisho huo kutimia baada ya staa huyo kutaka alipwe Pauni 13 milioni kwa mwaka.

Advertisement