Chelsea yampitia fasta Joao Pedro

Muktasari:
- Na The Blues pia ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa winga wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens kwa ada ya Pauni 55.5 milioni -- wakifanya matumizi yao ya uhamisho kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kufikia Pauni 212 milioni.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imevamia mawindo ya Newcastle United na kufanikiwa kunasa huduma ya Joao Pedro na imekubali kulipa Pauni 55 milioni kwenye dili la kumnasa mshambuliaji huyo wa Brighton.
Na The Blues pia ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa winga wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens kwa ada ya Pauni 55.5 milioni -- wakifanya matumizi yao ya uhamisho kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kufikia Pauni 212 milioni.
Pedro atawasili kwa ndege kutoka Brazil hadi Marekani kwenda kukamilisha vipimo vya afya, Jumanne. Na Chelsea ina matumaini kwamba mechi yake ya kwanza inaweza kuwa kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Palmeiras huko Philadelphia, Ijumaa.
Newcastle ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kunasa saini ya Pedro, lakini ada yao ya Pauni 50 milioni ilikataliwa. Lakini, Chelsea ilivamia na kufanikiwa kunasa huduma yake akiwa ni mchezaji ambaye kocha Enzo Maresca alimhitaji na kinachoelezwa, amepewa ofa ya mkataba wa miaka saba, huku ada yake, Pauni 50 milioni itatangulia kulipwa na Pauni 5 milioni itakuwa nyongeza.
Kinachoelezwa ni kwamba staa huyo wa Kibrazili mwenye umri wa miaka 23 alichokuwa akitaka ni kwenda kuichezea Chelsea na kitu kizuri Brighton imekuwa na uhusiano mzuri na The Blues.
Na sasa Chelsea imetumia Pauni 257 milioni kwenye ishu ya kuwasajili wachezaji Brighton tangu bilionea Todd Boehly alipochukua umiliki wa klabu hiyo ya Stamford Bridge miaka mitatu iliyopita.