Pep ashangilia ubingwa kwenye mgahawa wa staa wa Man United

Friday May 17 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

KIBONGO bongo ingekuwa noma na Pep Guardiola angeonekana kama anakwenda kuwasanifu tu mahasimu wake Manchester United baada ya kuipa Manchester City ubingwa wa Ligi Kuu England wakati wapinzani wake hao wakiwa wanapambana na hali yao.

Kilichotokea ni hivi, juzi Jumatano jioni, Guardiola aliwachukua wasaidizi wake kwenye benchi la ufundi huko Man City na kwenda nao kusherehekea ubingwa katika mgahawa mmoja unaomilikiwa na mchezaji wa Man United.

Cheki mabingwa wa Ligi Kuu England, Man City wanakwenda kusherehekea kubeba ubingwa huo kwenye mgahawa wa mchezaji wa Man United. Timu mbili zenye upinzani mkali huko jijini Manchester. Bosi huyo, Guardiola alipigwa picha akionekana akiingia katika mgahawa wa Tapeo & Wine unaomilikiwa na kiungo mchezeshaji wa Man United, Mhispaniola, Juan Mata.

Guardiola alivaa kawaida kabisa, suruali ya jinzi, raba nyeupe pamoja na sweta alipoonekana wakati akiingia kwenye mgahawa huo na wasaidizi wake huko Man City. Mgahawa huo wa Mata upo Deansgate jijini Manchester.

Kwa msimu huu, Guardiola na wasaidizi wake kwenye kikosi hicho cha Man City tayari wameshaipa mataji mawili ya ndani, Kombe la Ligi na Ligi Kuu England na kesho Jumamosi wataingia uwanjani kusaka taji lao la tatu la msimu huu watakapomenyana na Watford kwenye fainali ya Kombe la FA.

Advertisement

Kocha msaidizi, Brian Kidd alikuwa na Guardiola sambamba na Lorenzo Buenaventura, kocha wa utimamu wa mwili ‘fitinesi’ wa kikosi cha kwanza. Mark Sertori, mchua misuli naye alikuwamo kwenye mtoko huo sambamba na Guardiola, wakati Mikel Arteta alikwenda kujiunga nao baadaye kidogo.

Mata alianzisha mgahawa wake huo mwaka 2016 na bila shaka mashabiki wa Man City kuanzia sasa watakuwa wakienda hapo kwa wingi kupata mlo baada ya kuona benchi lao la ufundi lote likienda kupata mlo wa pamoja kushangilia mafanikio yao ya msimu katika mgahawa wa mchezaji wa Man United.

Mgahawa huo umedaiwa kuwa ni wa kiasili kabisa na wengi waliopata nafasi ya kwenda kula hapo walitoa ushuhudia wa misosi mitamu, ambapo kipa wa Man United, Mhispaniola David de Gea aliwahi kusema: “Napenda ukarimu na hali ya hewa ilivyo na chakula kilikuwa kitamu balaa.”

Guardiola ametoka na wasaidizi wake kwenda kupata mlo huo ambapo bila shaka utaambatana na mazungumzo ya namna ya kwenda kuwakabili Watford na kuzoa mataji yote ya soka la England kwa msimu huu.

Ushindi dhidi ya Brighton uliwafanya Man City kunyakua ubingwa wao wa pili mfululizo kwenye Ligi Kuu England Jumapili iliyopita ambapo lilikuwa taji lao la pili msimu huu na kesho wataingia uwanjani kuongeza taji la tatu.

Advertisement