Neymar pasua kichwa Barcelona

Monday June 24 2019

 

BARCELONA, HISPANIA

PHILIPPE Coutinho na Ousmane Dembele huenda wakatumika na Barcelona kama kete yao katika kumnasa Neymar kutoka Paris Saint-Germain ili kumrudisha Nou Camp, kwa mujibu wa ripoti zinavyodai.

Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu ameripotiwa na mpango wa kuwatoa mhanga washambuliaji hao wawili ili kufikia kiwango cha thamani ya pesa wanachotaka PSG ili kumwaachia Neymar.

Kwa mujibu wa Marca, PSG bado wanashikilia msimamo kwamba thamani ya Neymar ni Pauni 265 milioni kwa timu inayotaka ikilipa kiasi hicho cha pesa watakubali kuachana na staa wao. Kiwango hicho kipo mbali sana na Barcelona wanayotaka kulipa.

Hata hivyo, hawapo tayari kukata tamaa katika kukamilisha dili hilo, ambapo Bartomeu anaamini Neymar ana nguvu kubwa sana kwenye vyumba vya kubadilishia huko Nou Camp.

Hivyo, wanacheki uwezekano wa kumnasa Mbrazili huyo kwa kutoa kiasi kidogo cha pesa huku wakiwaweka kwenye dili wachezaji kadhaa.

Advertisement

Barca wanaweza kuwapa PSG pesa Pauni 45 milioni pamoja na wachezaji Dembele na Coutinho ili kumnasa Neymar. Lakini, dili jingine wanaloweza kufanya ni kutoa Pauni 130 milioni pamoja na mchezaji mmoja ama Dembele au Coutinho.

Dili jingine la tatu, Barca inaweza kutoka Pauni 90 milioni pamoja na mchezaji Dembele au Coutinho pamoja na Ivan Rakitic au Samuel Umtiti.

Hata hivyo, kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde, hayupo tayari kutumia nguvu nyingi katika kumrudisha Neymar huko Nou Camp kwa sababu anachotaka ni Dembele abaki kwenye timu yake.

Neymar aliachana na Barcelona miaka miwili iliyopita akihamia Paris Saint-Germain kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia ya Pauni 198 milioni.

Advertisement