Kuna dogo anataka jezi ya Hazard Chelsea

Friday May 17 2019

 

LONDON, ENGLAND

KINDA wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi ameripotiwa kutaka apewe jezi yenye namba 10 inayovaliwa na Eden Hazard kwenye timu hiyo ikiwa ni sehemu ya masharti yake ili asaini mkataba mpya wa kubaki Stamford Bridge.

Kinda huyo alikaribia kabisa kutimkia Bayern Munich kwenye dirisha la Januari, lakini Chelsea iliamua kumbakiza baada ya kutambua kwamba watakabiliwa na adhabu ya kufanya usajili.

Chelsea imefungiwa kusajili na sasa ipo kwenye wakati mgumu kumshawishi Hazard abaki kwenye timu yao baada ya kudaiwa kuwindwa kwa nguvu zote na Real Madrid. Ada ya Pauni 100 milioni imedaiwa inaweza kutoka kwa ajili ya kunasa huduma ya mchezaji huyo jambo linalomfanya Hudson-Odoi kutaka jezi yake kama ataondoka.

Kinda huyo alikuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kabla ya kupata majeraha yaliyosababisha afanyiwe upasuaji na kukosa msimu wote.

Hudson-Odoi kwa sasa jezi yake ina namba 20, lakini huko kwenye Twitter anatambulika kama @Calteck10. Kinda huyo anataka jezi yake ifanane na jina lake kwenye Twitter. Chelsea itasikiliza sharti lake kama Hazard ataondoka?

Advertisement

Advertisement