Juventus ipo siriazi na Pogba

Muktasari:

  • Klabu ya Juventus ipo mbioni kumrudisha kiungo wake wa zamani Paul Pogba baada ya supastaa huyo wa Ufaransa kuwa na wakati mgumu Old Trafford kutokana na kutibuana na Kocha Jose Mourinho.

TURIN, ITALIA. Juventus imeripotiwa kuanza mjadala wa kutazama uwezekano wa kumrudisha kiungo, Paul Pogba kwenye kikosi chake baada ya kuiuzia Manchester United miaka miwili iliyopita.

Bosi wa Juventus, Fabio Paratici amethibitisha kuwapo kwa mpango huo wa kumsajili Pogba baada ya supastaa huyo wa Ufaransa kuwa na wakati mgumu Old Trafford kutokana na kutibuana na Kocha Jose Mourinho.

Pogba aliondoka Juventus mwaka 2016 akirudi Man United kwa ada ya Pauni 89 milioni, ambayo ilivunja rekodi ya uhamisho kwa wakati ule, lakini mambo yake yamekwenda hovyo tofauti na alivyodhani baada ya kurudi kwenye Ligi Kuu England.

Pogba na Mourinho wapo kwenye uhusiano mbaya sana baada ya hivi karibuni kocha huyo kumsema mchezaji wake kuwa ni kirusi, anawaharibu wachezaji wengine kikosini.

Wakati dirisha la Januari likiwa karibu kufunguliwa, kumekuwa na ripoti Pogba anaweza kurudi zake Turin kwenda kuungana na Cristiano Ronaldo kwenye kikosi cha Juventus.

Kinachoelezwa Pavel Nedved amekuwa akishirikiana ana kwa ana na Kocha Massimiliano Allegri katika kuhakikisha Juventus inawanasa wachezaji inaowahitaji kwenye kikosi chake.

Pogba alicheza kwa miaka minne kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Serie A kabla ya kurudi England ambako awali aliwahi kucheza kwa muda mfupi kwenye kikosi cha Man United.