Guardiola kasema bado yupoyupo sana Etihad

Monday May 13 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

PEP Guardiola ameripotiwa kuwaambia mabosi wake huko Manchester City kwamba hajawahi kuwaza na wala hana mpango wa kuihama timu hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kwamba bado yupoyupo sana.

Kocha huyo Mhispaniola jana Jumapili alitarajia kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England katika kipindi cha muongo mmoja uliopita wakati kikosi chake cha Man City kilipomenyana na Brighton huko ugenini, huku wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Liverpool walikuwa na mchezo uwanjani Anfield dhidi ya wagumu Wolves.

Ubingwa wa ligi utawafanya Man City kujiweka kwenye nafasi bora kabisa ya kubeba mataji yote ya ndani ya England, kwani kabla ya hiyo jana ilikuwa tayari imeshabeba ubingwa wa Kombe la Ligi na imetinga fainali ya Kombe la FA.

Guardiola sasa amewatoa hofu mabosi wake kwa kuwaambia bado yupo sana kwenye kikosi hicho baada ya hivi karibuni kuwapo na uvumi kwamba kocha huyo amewekwa kwenye mipango ya Juventus wakimtaka mwishoni mwa msimu huu.

Kutokana na hilo, Juventus sasa wamehamishia nguvu yao kwa kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, ambaye wanamwona kuwa ni mtu sahihi wa kwenda kuchukua mikoba ya Massimiliano Allegri.

Advertisement