Emery imekula kwake kwa Mesut Ozil

Monday May 13 2019

 

LONDON, ENGLAND

KOCHA, Unai Emery inaelekea kula kwake baada ya supastaa Mesut Ozil kusisitiza kwamba hawezi kuondoka kwenye kikosi cha Arsenal mwishoni mwa msimu huu na kwamba atabaki Emirates hadi mwisho wa mkataba wake.

Kiungo huyo wa Kijerumani amekuwa kwenye mapito mengi chini ya kocha Emery, ambaye amekuwa akidai kwamba anapiga hesabu za kumuuza mchezaji huyo ili kupunguza bili ya mishahara kwenye kikosi chake.

Ozil, alisaini dili jipya linalomwingizia Pauni 350,000 kwa wiki kwenye kikosi hicho Januari mwaka jana wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya Arsene Wenger, lakini baada ya ujio wa Unai, mwanzoni mwa msimu ilionekana kama Mjerumani huyo anakwenda kufunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu. Lakini, sasa kiungo huyo haonekani kuwa na mpango wa kuondoka akipanga kubaki hapo akivuna mshahara wake mnono hadi mwisho wa mkataba wake.

Wakala wake, Dr Erkut Sogut amesema wazi kwamba hakuna mpango wowote wa mteja wake kuondoka kwenye timu hiyo na Ozil mwenyewe alisema: “Nimebakiza miaka miwili kwenye mkataba wangu. Sielewi kitakachotokea baada ya hapo, lakini kwa wakati huu siendi kokote.” Mkataba wa Ozil kwenye kikosi hicho cha Arsenal utafika tamati 2021.

Advertisement