Bakayoko, Fabinho, Mbappe wamng’oa kocha

Muktasari:

  • Timu ya Monaco FC ya Ligi Kuu Ufaransa, imejiingiza matatizoni kutokana na uamuzi wake wa kuwauza wachezaji wake nyota watano kati ya walioipa ubingwa misimu miwili iliyopita. Katika mkakati wa kujinasua mkiani katika msimamo wa Ligi na kukwepa kushuka daraja, imepanga kumpa Thierry Henry nafasi ya kocha Leonardo Jardim ambaye wamepanga kumtimua kwa dhana kuwa ndiye aliyeshindwa kuipa mafanikio msimu huu.

Monaco, Ufaransa. Klabu ya Monaco inajutia uamuzi wa kuwauza wachezaji wake nyota Tiemoue Bakayoko, Fabinho, Thomas Lemar, Kylian Mbappe na Benjamin Mendy.

Klabu hiyo imepanga kumalizia hasira zake kwa kumtimua Kocha wake Leonardo Jardim, aliyewapa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2016/2017 kutokana na matokeo duni.

Monaco iliwaachia wachezaji hao kwenda timu mbali mbali baada ya kuchangia mafanikio makubwa na sasa imejikuta kwenye janga la kupigania kutoshuka daraja badala ya kuwazia ubingwa, kwani ipo nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi sita katika mechi tisa pointi 21 nyuma ya vinara PSG.

Mbappe amekuwa muhimili wa mabao PSG, Fabinho anaing’arisha Liverpool, Mendy alianza vizuri Manchester City, Lemar anang’aa Atletico Madrid na Bakayoko yupo Chelsea ingawa hajawa na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

Klabu hiyo imemuangukia mshambuliaji wake wa zamani Thierry Henry, ambaye ameshaanza mazungumzo ya kuinoa Aston Villa, arejee nyumbani kuokoa jahazi kutokana na nafasi waliyopo.

Henry kinara wa ufungaji wa muda wote katika timu ya Taifa ya Ufaransa, aliichezea Monaco mechi 141 kabla ya kutua Arsenal, alikopata mafanikio makubwa kisoka.

Kwa sasa Henry ni Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Ubelgiji akiwa na jukumu la kuwanoa washambuliaji na mfumo mzima wa utafutaji mabao.

Henry alikuwepo Monaco mwezi uliopita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushuhudia timu hiyo ikilala kwa mabao 2-1 kutoka kwa Atletico Madrid ya Hispania.

Monaco imeshindwa kupata ushindi katika mechi kumi mfululizo za michuano mbali mbali huku ikipoteza mechi nne mfululizo matokeo ambayo ni mabaya zaidi katika historia ya klabu hiyo.