Ziyechi wa Pauni 38 milioni,Sancho wa Pauni 120 milioni

Muktasari:

Sancho amecheza mechi 53, sita zaidi ya alizocheza Ziyech huko Ajax, aliyecheza mechi 47.

LONDON,ENGLAND . VITA kubwa itakwenda kuibuka mwisho wa msimu kuwania huduma ya Jadon Sancho. Kiwango chake bora ndani ya uwanja kinavutia timu nyingi, huku Manchester United wakiwa tayari kuvunja kibubu kutoa Pauni 120 milioni ili kunasa huduma ya kinda huyo wa Kingereza.

Wakati Man United wakisubiri kutumia mkwanja wa Pauni 120 milioni, Chelsea wao wameshajichukulia Hakim Ziyech wa kiwango kama kilekile cha Sancho, lakini kwa pesa ndogo zaidi ya theluthi moja. Chelsea walikuwa wakimtaka pia Sancho wa Borussia Dortmund, lakini kitu hicho kinaweza kisitokee tena baada ya kufikia makubaliano na Ajax kuhusu kumnasa Mmorocco na kwamba, atatua Stamford Bridge mwishoni mwa msimu. Mastaa hao wawili yupi mwenye huduma bora ukimleta kikosini. Hizi hapa data za wachezaji hao wawili wanaofanana nafasi zao za kucheza ndani ya uwanja, ila mmoja wa bei mbaya, mwingine wa bei chee!

Sancho amecheza mechi 53, sita zaidi ya alizocheza Ziyech huko Ajax, aliyecheza mechi 47.

Kwenye mechi hizo, Sancho ameanzishwa mara 44, wakati Ziyech ameanza mechi zote 47.

Kwa ujumla wa dakika walizokuwa ndani ya uwanja, Sancho amecheza dakika 3,999, wakati Ziyech amecheza dakika 3,835. Katika dakika hizo walizocheza, Sancho amefunga mabao 24 na Ziyech mabao 22, huku Sancho akiwa na asisti 27 na Ziyech asisti 25.

Sancho amehusika kwenye mabao 51 na kupiga mashuti 77, wakati Ziyech amehusika kwenye mabao 47 na kupiga mashuti 239. Kwenye mashuti hayo, Sancho amelenga goli mara 43, wakati Ziyech amelenga goli mara 89. Staa Sancho ametengeneza nafasi za mashambulizi 111 ikiwamo asisti, wakati Ziyech ametengeneza nafasi 173. Ni huduma karibu zinazofanana, lakini Ziyech amekubaliwa kujiunga na Chelsea kwa Pauni 38 milioni tu, huku Sancho ikihitajika kulipwa Pauni 100 milioni zaidi kwenye dili hilo linalompeleka Ziyech Stamford Bridge.