ZigZaga:Shujaa aliyeinusuru Simba kushuka daraja ageuka dereva

Muktasari:

 Watu wa Simba walitulia kwenye majukwaa ya Uwanja wa Taifa mioyo ikiwadunda kuisubiri ‘dabi’ hiyo iamue hatima yao kwenye ligi, huku Yanga ikiwa na matumaini ya kutangaza ubingwa siku hiyo kwa vile sare ilitosha kuipa ndoo hiyo. 

Babati. WAKATI Simba leo ikijivunia straika, Meddie Kagere, aliyefanya vitu vikubwa na kuisaidia timu kutwaa ubingwa wake wa 20 wa Ligi Kuu ya Bara na kufika robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ulioisha, kuna jambo ambalo baadhi ya mashabiki hawalifahamu.

Pengine Simba isingekuwa katika nafasi hii iliyopo sasa kama si mambo makubwa yaliyofanywa na John Makelele ‘ZigZaga’.

Huyu ndiye shujaa mwokozi wa Simba.

Ukiiona Simba ya sasa inakula raha za mafanikio, unaweza usifuatilie historia yake. Simba imeshapitia katika vipindi vigumu kadhaa na kimojawapo ni mwaka 1989 ilipokaribia kushuka daraja.

Stori kubwa mtaani wakati huo zilikuwa ni jinsi ambavyo Simba itashiriki Ligi Daraja la Pili msimu wa 1990. Wengi walipoteza matumaini ya kubaki katika Ligi Kuu (wakati huo ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza).

Kilichowakatisha tamaa wengi Simba ilikuwa imebakisha mechi moja ili kumaliza msimu na ilikuwa ni lazima ishinde mechi hiyo ili kunusurika kushuka daraja.   Kukawa na tatizo kubwa mbele yao. Yanga.

Mechi hiyo ya mwisho ilikuwa ni dhidi ya Yanga baada ya kutoka kufungwa 1-0 na Pamba ya Mwanza.

Kikwazo kilikuwa ni viwango vya ubora baina ya timu hizo kwa wakati huo.

Wakati Simba ‘iliochoka’ ilikuwa ikihitaji kushinda mechi hiyo ili kunusurika kushuka daraja, Yanga ilikuwa katika ubora wake ilihitaji sare tu katika ‘dabi’ hiyo ya Kariakoo kwenye Uwanja wa Taifa (siku hizi Uhuru) ili kutwaa ubingwa.

Mashabiki wenye roho nyepesi wa Simba hawakuthubutu hata kwenda uwanjani.

Wale wenye mioyo ya chuma walijikongoja kinyonge kwenda uwanjani ambako mashabiki wa Yanga walikuwa na mzuka wa ajabu wakijiandaa kubeba ndoo.

Watu wa Simba walitulia kwenye majukwaa ya Uwanja wa Taifa mioyo ikiwadunda kuisubiri ‘dabi’ hiyo iamue hatima yao kwenye ligi, huku Yanga ikiwa na matumaini ya kutangaza ubingwa siku hiyo kwa vile sare ilitosha kuipa ndoo hiyo.

Filimbi ikapulizwa. Yanga kama ilivyotarajiwa ilianza kwa kujiamini kwa sababu katika mechi hiyo Simba ilikuwa ‘underdogs’.

Lakini mambo yalianza kubadilika dakika 21. Edward Chumila akatupia bao la kuongoza lililoivuruga Yanga na kuamsha shangwe si la kitoto katika majukwaa ya mashabiki wa Simba.

Hata hivyo, Yanga haikukubali. Ikachomoa bao hilo kupitia kwa Issa Athuman katika dakika ya 36 na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa.

Kipindi cha pili ndipo John Makele Zigzag alipotengeza historia ambayo itadumu kwa vizazi na vizazi katika Klabu ya Simba na soka la Tanzania kwa ujumla. Straika huyo ambaye siku hiyo alisimama namba tisa, alifunga goli matata katika dakika ya 58 lililoweka rekodi ya aina yake.

Mashabiki walishusha shangwe la nguvu ambalo lingeweza kuezua paa baada ya bao hilo lililompa Mnyama ushindi wa 2-1 uliowabakiza kwenye Ligi Kuu huku Yanga ikipokonywa ubingwa ambao ulienda kwa Coastal Union ya Tanga.

Bao hilo ndilo limemfanya Zig-zaga kuandika historia ya kipekee kwanza kuikomboa Simba, pili ndiyo lilikuwa bao lake pekee kuifunga Yanga akiwa na Simba kwani bao lake la kwanza kuifunga Yanga ilikuwa mwaka 1987 akiwa na Pamba pale CCM Kirumba Mwanza.

SAHAU SIMBA, YANGA KUSHUKA DARAJA

“Kuna vitu vingi nyuma ya pazia juu ya timu hizi hasa kwa viongozi yaani bora Yanga au Simba isichukue ubingwa kuliko timu mojawapo ishuke daraja,” anasema Makelele.

Mkongwe huyo anaeleza kuna sababu nyingi zinazosababisha timu kongwe na wapinzani wa siku nyingi, Simba na Yanga kuwa haziwezi kushuka daraja kirahisi kutokana na mifumo ya soka ilivyo.

“Simba na Yanga ndiyo wanaobeba soka la Tanzania tangu enzi na kuna heshima yake na mbaya zaidi viongozi wa soka nao ni wapenzi na wanachama wa timu hizo.

“Usishangae kukuta kiongozi wa timu ya Ndanda SC au Singida United kuwa mpenzi na mwanachama wa Yanga, hivyo kwao ni vyema timu zao zikafungwa kuliko kuiona Yanga au Simba ikifungwa.”

Zig-zaga anasema: “Simba inaweza kwenda Arusha kucheza dhidi ya timu ya Arusha lakini wanachama wataiacha timu ya mkoa wao wakaigeukia Simba au Yanga na kuzipa mapokezi makubwa na kuisahau timu yao.”

AWA DEREVA WA SIMBA

“Nilikuwa napenda sana kazi ya kuendesha gari, lakini sio kwamba nilikuwa dereva wa Simba, bali nilikuwa namsaidia dereva wakati wa safari ndefu na aliniamini kila mara nilifanya hivyo kwa mapenzi yangu na si kulazimishwa,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza hata Chumila naye alikuwa anaendesha gari la timu wakati wakiwa wanaelekea mikoa ya mbali kama vile Mbeya na Songea kwa kuwa dereva alikuwa mmoja, hivyo alikuwa anachoka kuendesha peke yake.

JINSI ALIVYOANZA SOKA

Hakuna aliyemshawishi kuingia kwenye soka, zaidi ya kuona mastaa kadhaa wakikipiga kwenye timu mbalimbali ndiyo sababu iliyomfanya azame kwa miaka 12 kwenye soka.

“Nilipenda sana mpira na sikuwa na mawazo yoyote ya kufanya kazi nyingine ndiyo maana niliweka nguvu nyingi kwenye mpira, kila wakati nilikuwa nafanya mazoezi.

“Enzi zetu wachezaji walikuwa wanajitambua vilivyo kwani tuliheshimu vipaji vyetu japo kulikuwa hakuna malipo yoyote ndiyo maana maisha ya wengi hayapo sawa.

“Tulikuwa tunategemea zaidi viingilio vya mlangoni pamoja na wadau, hivyo siku mkifanya vizuri, basi mnapewa pesa nzuri japo ilikuwa siyo ya kukufanya ufike mbali katika malengo ya kujenga maisha yako.”

PAMBA ILIVYOMNASA

Baada ya kuanza vyema soka lake la mchangani akiwa na TPC ya Kilimanjaro iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Tatu kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1984 alitimkia Ushirika Moshi.

Akiwa na Timu ya Ushirika Moshi walifanya mambo mengi makubwa ikiwamo kubeba taji la Ubingwa wa Mkoa mwaka 1985 pamoja na ubingwa wa kanda katika Kituo cha Kilimanjaro.

Mwaka mmoja baadaye Pamba ilivutiwa na huduma yake ikafanya jitihada na kuinasa saini yake na kumhamisha makazi na maisha mapya yakaanza akiwa na Pamba SC jijini Mwanza.

Makelele aliwasha moto kwelikweli akiwa na Pamba iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) kiasi cha kuwakuna vigogo wa  Simba kabla ya kurejea tena mwaka 1991 japo hakudumu sana kwani mwaka uliofuata aliachana na soka rasmi na kugeukia kazi ya udereva.

Aliitumikia Pamba kwa miaka miwili tu kwani mwaka 1988 alihamia Simba ambayo huko akaendeleza moto kama kawa kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Majanga yakaanza Msimbazi akiwa ndiyo kwanza anatua hapo, kikosi hicho kilikuwa kinashuka daraja na mchezo wa mwisho ulikuwa dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, ambao nao walikuwa wakihitaji ushindi ili kubeba ubingwa.

“Kabla ya kukutana na Yanga tulitoka kukipiga dhidi ya Pamba huko mambo yakawa siyo mzuri kwani tulifungwa bao 1-0, hivyo tukapiga kambi ya siku tatu mkoani Dodoma.

“Hapo kazi kubwa kwa viongozi ilikuwa ni kutupa ushauri na kututia moyo juu ya kuinusuru Simba isishuke daraja, kwani kila mtu alijua Simba inakwenda kupotea kwasababu Yanga ilikuwa vizuri kwelikweli,” anasema kuhusu mechi hiyo aliyofunga goli la ushindi wa 2-1 na kuibakisha Simba kwenye Ligi Daraja la Kwanza ( sasa Ligi Kuu).

HUYU BEKI ALIMSUMBUA SANA

Kati ya mabeki ambao Zig-zaga hataweza kuwasahau katika maisha yake ya soka ni pamoja na kisiki cha Yanga, Godwin Aswile ‘Scania’, ambaye alikuwa hawezi kumwacha hata hatua moja.

“Yanga ni timu ya tofauti, kwani asili yao ni soka la jihadi tangu miaka ya nyuma, wanatumia nguvu na hata asilimia kubwa ya wachezaji wao huwa hivyo.

“Aswile alikuwa hataki kuona nikishika mpira hata kwa sekunde kadhaa, alikuwa akinitibulia kila wakati na jinsi alivyokuwa anacheza ilinifanya niwe makini dhidi yake.”

JINA ZIGZAGA LILIVYOKUJA

Kila kitu kinakuja na maana yake iwe mbaya au nzuri hii inatokana na jinsi matendo ya mtu yalivyo lakini Makelele anaeleza jina la Zig-zaga lilitokana na jinsi alivyokuwa akiwachambua mabeki wa timu pinzani.

“Zile chenga zangu za kupiga kona kama umbo la zig-zag, basi ziliwafanya mashabiki wa Pamba kuniita Zig-zaga kila mara na kuanzia hapo hata wachezaji wenzagu wakawa wananiita hivyo.”

ANAVYOMKUBALI COULIBALY

Zig-zaga anasema kikosi cha Simba kimekamilika kila eneo ni makosa madogomadogo ambayo yanapaswa kuangaliwa japo si tatizo kubwa sana kwani kila timu haikosi upungufu, huku akimkubali beki wa kulia Zana Coulibaly, licha ya mashabiki wengi wa Simba kutilia shaka uwezo wake.

“Huyu mchezaji wakati anatua nchini wengi walimponda kutokana na mambo yake haya ya ujana, lakini kocha ndiye aliyekuwa anamjua vyema na sasa kila mmoja anakubali Zana kuwa ni kati ya wachezaji wazuri.

“Mchezaji huwezi kumtazama kwenye mchezo mmoja, lazima akae na kuzoea mazingira pamoja na mfumo wa kocha ndiyo maana hata, Clatous Chama pamoja na Haruna Niyonzima nao wamekuwa msaada mkubwa kwenye timu baada ya kukaa kwa muda japo Niyonzima awali mambo yalikuwa siyo mazuri kwake.