Zahera: Timu nyingi zinanitaka

Muktasari:

Akizungumza jana, Zahera alisema hana hofu ya kupoteza kazi kwa kuwa ana idadi kubwa ya klabu zinazomtaka ingawa hakutaka kuzitaja kwa majina.

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Yanga kung’olewa katika mashindano ya kimataifa, kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera amesema ana ofa nyingi mkononi kutoka kwa klabu zinazomtaka.

Yanga imeaga mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 3-0 na Pyramids ya Misri, juzi usiku. Katika mechi ya kwanza ilichapwa 2-1 mjini Mwanza.

Akizungumza jana, Zahera alisema hana hofu ya kupoteza kazi kwa kuwa ana idadi kubwa ya klabu zinazomtaka ingawa hakutaka kuzitaja kwa majina.

Zahera alitoa jibu hilo baada ya mwandishi wa gazeti hili kumuuliza iwapo yupo tayari kuwajibika baada ya Yanga kutolewa katika hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 5-1.

“Sina tatizo, hata kama leo nikiondoka Yanga kesho nitapata timu nyingine kwa sababu zipo timu nyingi zinanitaka. Kuna nchi nyingi zinahitaji makocha wakubwa kama mimi, siwezi kupata shida,” alisisitiza kocha huyo raia wa DR Congo.

Hata hivyo, Zahera alisema hakuna kiongozi aliyewahi kumtamkia suala la kusitisha mkataba wake ambao unatakiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Wakati Zahera akitoa kauli hiyo, taarifa za ndani zinasema kocha wa zamani wa timu hiyo Hans van der Pluijm ameteta na baadhi ya vigogo wa klabu hiyo wakitaka kumrejesha.

Pia aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Kim Poulsen ni miongoni mwa majina yanayotajwa kuchukua nafasi ya Zahera endapo ataondolewa.

Hata hivyo, Zahera alisema baada ya kuondolewa katika mashindano ya kimataifa akili yake anaielekeza kwenye michuano ya Ligi Kuu na ataanza na mchezo dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

“Niwaondoe presha mashabiki wa Yanga bado nafikiria kuitumikia timu hii ambayo nina imani msimu huu ni bora zaidi ya vile ambavyo ilikuwa msimu uliopita,” alisema.