Zacharia : Nasubiri Amunike aniite Stars

Monday January 14 2019

 

By Eliya Solomon

YALE maneno ya wahenga kuwa mkataa kwao ni mtumwa yameendelea kuishi kwa hata wanasoka wa Kitanzania ambao waliondoka nchini na kwenda kutafuta mafanikio ya soka la kimataifa katika ligi zilizoendelea hasa kule Ulaya.

Wanasoka hao wamekuwa na utayari wa kukipiga kwenye Timu ya Taifa na wengi wao wameonekana kuwa wazalendo kwa kukataa kubadilisha uraia wao hata pale walipo shawishiwa na mataifa ya ligi wanazozichezea.

Hakika maneno ya wahenga yamekuwa na tija kwa wachezaji hao ambao wengi wao wameonekana kutotaka kuwa watumwa katika mataifa yasiyowahusu.

Zakaria Kibona Anayeichezea IF Gnistan ya Ligi Daraja la Pili Finland ni miongoni mwa nyota wa Tanzania ambao wamegoma kutumika kwenye timu za mataifa ya ligi wanazocheza.

Kibona amezungumza na Nje ya Bongo moja kwa moja kutoka kwenye Mji wa Helsinki ambapo inapatikana timu yake na kuweka wazi kuwa muda wowote atajumuika na timu ya taifa kama Kocha Emmanuel Amunike atamjuisha kwenye kikosi chake.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, msimu uliomalizika mwaka jana amefunga mabao matatu kwenye michezo 13 ya Ligi Daraja la Pili Finland.

“Nimefurahi sana, nilikuwa sina mawasiliano baina yangu na watu wa Tanzania na ndiyo maana nilipoteza imani ya kuitwa timu ya taifa, lakini kunifuatilia kwenu watu wa Mwananchi naamini Kocha Emmanuel Amunike ataniita.

“Wakati ninaanza kucheza soka huku nilikuwa nawaza ni muhimu nikipata uzoefu niutumie kwa kulitumikia taifa langu la Tanzania, nimekutana na makocha wengi wenye uwezo wa juu ndiyo maana nimekuwa nikifunga mara kwa mara kama mshambuliaji.

“Tanzania kwangu ni kama mama, nimekuwa nikipenda kusema mama huwa ni mama kwa mtoto wake, hata iwaje siwezi kumkana mama yangu hata kama nikikosa nafasi ya kuichezea timu ya taifa,” anasema mshambuliaji huyo.

Hata hivyo, Kibona alidai aliwahi kuonja kuvaa uzi wa timu ya taifa lakini ilikuwa ni kwa upande wa vikosi vya vijana ambao walikuwa chini ya miaka 17.

“Mwaka 2006 nilikichezea kikosi cha Serengeti Boys, kipindi hicho nilikuwa mdogo na uwezo wangu wa kufunga ulianzia hapo kwa sababu haikuwa inapita michezo mitatu bila ya kufunga mabao nadhani kwa niliocheza nao wanaweza kunikumbuka.

“Kutokana na masuala ya kuhitaji zaidi mafanikio ilibidi nije huku ili kupigania ndoto yangu ya kuwa mchezaji wa kulipwa.” anasema.

Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Machi 14, 1990 jijini Dar es Salaam alianza maisha yake ya soka kwenye timu ya Ligi Daraja la Pili Finland iitwayo Atlantis FC kama mchezaji kijana na baadaye alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza.

“Nilicheza Atlantis lakini kama unavyojua maisha ya mpira nikahama na kwenda kujiunga na Kubi O4, niliichezea hiyo timu kwa msimu mmoja tu wa 2009/2010.

“Nilihama tena hapo na kwenda PK-35 na kucheza msimu mmoja na 2011/2012 nilikuwa nimeamia Mosta FC sikuwa nadumu kwenye timu moja maana nilikuwa nicheza huku kwa kiwango wengine wanavutia na kiwango changu.

“Zingine nilizozichezea ni Helsinki IFK, FC Viikingit, BK-46, FC Legirus na PK-35 Vantaa,” anasema Kibona.

Hata hivyo, Kibona alidai nchi hiyo yenye mastaa kama Roman Eremenko wa CSKA Moscow ya Urusi na Teemu Pukki wa Brondby ya Denmark ni moja ya mataifa yanayo thamini vipaji vya vijana.

“Wanaufutiliaji wa maendeleo ya vijana kwa karibu sana tofauti na mataifa mengi ya Afrika nadhani kama tukibadilika kwenye hilo linaweza kutusaidia,” anasema.

Wasifu wake

Jina Kamili: Zakaria Kibona

Kuzaliwa: Machi 14, 1990 (28)

Mahali: Dar es Salaam, Tanzania

Timu: IF Gnistan

Nafasi: Straika

Advertisement