Yondani, Fei Toto hawapoi Jangwani

Muktasari:

  • NYOTA wa Yanga akiwamo Kelvin Yondani waliokuwa katika timu ya taifa, Taifa Stars iliyonyukwa bao 1-0 na Lesotho, jasho likiwa halijawakauka wameunganishwa kwenye safari ya klabu yao kwa mechi za viporo Kanda ya Ziwa.

NYOTA wa Yanga, Kelvin Yondani, Feisal Salum ‘Fei Toto’ hakuna kulala wala kupoa kwani baada ya majukumu yao ya timu ya taifa, wanatarajiwa kuungana na nyota wengine leo Jumanne ili kuifuata Mwadui FC ya Shinyanga kwa mchezo wao wa kiporo cha Ligi Kuu Bara kitakachopigwa Alhamisi hii.

Nyota hao walikuwa na Stars katika pambano lao la kuwania Fainali za Afcon 2019 dhidi ya Lesotho na kupoteza, hivyo hawatakuwa na mapumziko kwa vile Yanga inawahitaji kusaka ushindi katika mechi yao ya kwanza ugenini.

Mbali na nyota hao, pia beki Gadiel Michael na kipa Beno Kakolanya waliokuwa na Stars wataungana sambamba na Kocha Mwinyi Zahera ambaye kwa pamoja wametua usiku wa kuamkia leo na kwenda moja kwa moja Kanda ya Ziwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh mara baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao Namungo ulioisha kwa sare ya bao 1-1 ilirudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ratiba nyingine.

Hafidh alisema wataondoka kwa usafiri wa anga ili kutowachosha wachezaji wao ambapo watazunguka Mwanza kabla ya kwenda Shinyanga na baadaye Bukoba kwa ajili ya mechi yao na Kagera Sugar itakayopigwa Jumapili ya wiki hii.

“Nyota waliokuwa na timu Taifa Stars hawawezi kupewa muda wa mapumziko kwasababu mchezo wetu na Mwadui upo karibu sana na hauwezi kusogezwa mbele kutokana na kuwa mchezo wa kiporo tutapanda ndege kuwapunguzia uchovu,”

“Hata waliokuwa hawajaungana na timu ya taifa pia wana uchovu kwani juzi tumecheza mechi tumesafiri siku inayofuata tena kwa basi hata hatujapumzika

tunaanza safari tena kikubwa tunachokiangalia ni kuwahi kwa kutumia usafiri wa anga ili wachezaji wakifika waweze kufanya mazoezi ya viungo na utimamu wa mwili na kesho waingie uwanjani kusaka pointi tatu muhimu,” alisema.

Akizungumzia majeruhi waliowaacha Dar es Salaam, Hafidh alisema Juma Mahadhi tayari ameanza mazoezi mepesi baada ya kukaa nje kwa muda mrefu na Papy Tshishimbi pia bado yupo katika uangalizi wa daktari.

“Majeruhi hawawezi kuwa miongoni mwa nyota tutakaosafiri nao kutokana na kuwa chini ya uangalizi kabla hawajaruhusiwa kuungana na wenzao kwa ajili ya mazoezi,” alisema.