Yanga yatua, Ajib...

Monday April 16 2018

 

WELAYTTA Dicha ya Ethiopia wana taarifa kuwa, wapinzani wao Yanga tayari wameingia ndani ya ardhi yao kule Awassa. Yanga imetumia nusu siku kusafiri kutoka jijini Dar es Salaam na kutua Ethiopia, lakini wakati safari hiyo inaanza mshambuliaji wake Ibrahim Ajib akashtua watu baada ya kukosekana.

Hata hivyo, taarifa zikadai kuwa Ajib amechwa kutokana na kuugua ghafla. Mbali na Ajib pia Yanga imemwacha beki Andrew Vicent ‘Dante’ ambaye aliumia katika mchezo wa kwanza wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi Dicha na ameshindwa kupona kwa wakati.

Safari ilivyokuwa

Mpaka inafika jijini Awassa Yanga ilitumia saa tisa njiani ambapo, kati ya hayo manne pekee ndiyo yaliyotumika angani wakitumia saa mbili kutoka Dar es Salaam kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata, Kenya.

Kutoka hapo ilitumia saa zingine mbili kuwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia safari hiyo wakitumia ndege ya Shirika la Kenya.

Wazuiwa saa tatu

Ilipofika Uwanja wa Bole, Yanga ililazimika kupoteza saa tatu uwanjani hapo wakisubiri nyaraka za majina ya msafara wake ambao maafisa hao wa uhamiaji walikuwa na majina ya watu 21 pekee.

Mpaka inafika hapo Yanga ilikuwa na msafara wa watu 35 na timu pekee ilikuwa na watu 25 na viongozi watano huku mashabiki na wadau wao wachache wakifikisha watu 35.

Safari ya basi yaanza

Mabosi wa timu hiyo walifanya maamuzi magumu kwa kuisafirisha timu hiyo kwa usafiri wa basi baada ya kuambiwa hakuna ndege katika siku ya Jumapili itakayowapeleka jijini Awassa ambapo mchezo huo utapigwa na kupiga hesabu za haraka.

Viongozi hao wakingozwa na mkuu wa msafara wa klabu hiyo, Salum Mkemi na Mkuu wa Msafara kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Lameck Nyambaya walilazimika kubadili akili wakishirikiana na Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani aliyetangulia mapema nchini hapa ambaye tayari alishandaa basi la kisasa lililotumika kuipeleka timu hiyo Awassa.

Kikosi hicho licha ya wachezaji kuonyesha kuchoka kilitumia saa matano kusafiri kwa basi na kufika Awassa na kuweka kambi katika hoteli moja ya kisasa ya Rori iliyopo hatua 45 kufika uwanja ambao, utatumika kuchezewa mechi ya Aprili 18.

Hata hivyo, kitendo cha kusafiri kwa basi Yanga illazimika kuvunja ratiba yao ya awali ya kufanya mazoezi siku ya jana jioni baada ya kufika wakiwa wamechelewa huku pia wachezaji wao wakionekana kuelemewa na uchovu.