Yanga yafumua benchi, yabakiza Wasauzi

Muktasari:

Klabu hiyo jana Agosti 3, 2020 ilipunguza wachezaji 14 na kuwaacha 17 ambao wataungana na wachezaji wapya watakaosajiliwa

YANGA imepitisha fagio lingine la chuma ikiwaondoa wazawa wote katika benchi lao ufundi na kubakiza wawili tu raia wa kigeni kutoka Afrika Kusini.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kumpiga chini Kocha Mkuu, Luc Eymael kwa tuhuma za ubaguzi.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominick Albinius leo imesema kuwa baada ya kufumua kikosi chao wakiwaondoa wachezaji 14 sasa wamefanya mabadiliko pia katika benchi lao la ufundi.

Katika mabadiliko hayo Yanga imewaondoa makocha wawili,daktari mmoja aliyeomba kupumzika,meneja wa timu na mtunza vifaa ambapo nafasi hizo sasa zitajazwa upya.

Albinius alisema aliyekuwa kocha wao msadizi wa kwanza Charles Mkwasa amemaliza muda wake na atapumzika sambamba na kocha wa makipa Peter Manyika.

Wengine ni aliyekuwa meneja wa kikosi chao Abeid Mziba na mtunza vifaa Fred Mbuna wote wamebadilishiwa majukumu yao ndani ya klabu hiyo huku daktari wa timu hiyo Sheick Mngazija naye akiomba kupumzika.

"Katika mabadiliko hayo,aliyekuwa kocha wetu msaidizi Charles Mkwasa amemaliza muda wake na tumekubaliana kwamba atapumzika,kocha wa makipa Peter Manyika,meneja wa timu Abeid Mziba na mtunza vifaa Fred Mbuna wote watabadilishiwa majukumu,"amesema Albinus.

"Klabu inatoa shukrani kwao kwa muda wote kwa muda ambao wamehudumu katika nafasi zao,hawa bado ni wenzetu lakini kutokana na sababu mbalimbali kama ambavyo nimeeleza tumefikia makubaliano hayo."

Albinius alisema kuwa katika mabadiliko hayo hayatawakumba watu wawili kocha msaidizi wa viungo Reidoh Berdien na daktari wa viungo Fareed Cassim Ambao ni raia wa Afrika Kusini.

"Kwenye timu ya wakubwa tutaendelea kuwa na kocha msaidizi Reidoh Berdien na daktari wa viungo Fareed Cassim ambao wataungana na kocha mpya na watendaji wengine watakaotangazwa hapo baadaye."

Kwa taarifa za kina kuhusu usajili usikose kusoma gazeti la Mwanaspoti kesho Agosti 5, 2020…