Charles Hilary azikwa kwao Zanzibar, wakongwe wamlilia

Muktasari:
- Charles alizaliwa October 22,1959 katika Mtaa wa Jang'ombe na kukulia Makadara Mjini Zanzibar na kufariki dunia Mei 11, 2025 katika Hospital ya Mloganzila jijini Dar salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Unguja. Wakati safari ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Charles Hillary ikitamatika rasmi kwa kupumzishwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe Mjini Unguja, baadhi ya waandishi na watangazaji wakongwe wamemzungumzia kama mtu aliyekuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya habari.
Charles alizaliwa October 22,1959 katika Mtaa wa Jang'ombe na kukulia Makadara Mjini Zanzibar na kufariki dunia Mei 11, 2025 katika Hospital ya Mloganzila jijini Dar salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Charles aliyekuwa Nguli katika Utangazaji na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Desemba 30, 2021, kisha kuteuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Februari 6, 2023 aliwahi kuwa mtangazaji wa vyombo vya habari mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania.

Mwandishi wa habari na Mtangazaji Mkongwe, Tido Mhando amesema leo imekuwa ni siku ngumu kwake kwani alifanya naye kazi kwa muda mrefu na ndiye aliyemshawishi kutoka Ujerumani kwenda London kujiunga na Idhaa ya Kiswahili BBC na kumtoa huko kujiunga na Kampuni ya Azam Media.
"Wakati mimi nafanya kazi Redio Tanzania Charles alikuwa shule ila kitu ambacho kilikuja kunishangaza aliponiambia kuwa alikuwa ananifatilia na alidhirisha hilo aliponiimbia wimbo ambao naucheza kama kuanzishia ripoti yangu na hapo ndipo nilipoamini kuwa kweli alikuwa ananifatilia," amesema Tido
Naye, Mtangazaji kutoka Azam, Ivona Kamuntu amesema licha ya tasnia ya habari kutikisika kwa kuondokewa lakini Azam imeguswa zaidi kwani alikuwa mlezi wa Kampuni hiyo wakati wote.
Ivona amesema ataendelea kusherehekea maisha yake kama zawadi ya pumzi ya uhai katka mambo makuu manne ikiwemo nidhamu ya kazi, furaha, kuwa na hamu ya kufanya vizuri na kutumia lugha ya Kiswahili ipasavyo.

Amesema, Licha ya kuwa Mkurugenzi wa Redio ya UFM bado alimuheshimu kila mmoja na nidhamu hiyo ameijenga kwa kila mtu na aina ya rika
Farouk Kareem amesema wakati anafanya kazi naye awali hakujua kuwa ni Mzanzibar baada ya miaka kupita na kumuhimiza lazima awe anapeleka habari kutoka Zanzibar katika mazungumzo yao siku moja ndipo alipomweleza kuwa alizaliwa kisiwani humo.
Farouk amesema waandishi wa habari Zanzibar watamkumbuka mpendwa huyo kwa kuwajengea daraja baina ya waandishi na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kutengeneza mfumo wa kukutana naye na kuwa huru kuuliza maswali wanayotaka.
Farouk amesema watalienzi daraja hilo ambalo wametengenezewa na wataishi kwa kukumbuka fikra, busara na maono yake.
Kwa upande wake, Maulid Kitenge amesema mwaka 1999 aliajiriwa na Charles Redio One kwa kuona kipaji chake na kuridhia kufanya naye kazi.

Amesema, kati ya vitu ambavyo anavikumbuka kutoka kwake ni kuwakosoa katika hali ya utani na hata alipoondoka aliendelea kuwathamini na kuwasikiliza.
"Mimi ni kijana niliyepikwa na yeye mwenyewe mkoni na kunikadhibidhi kwa Abuubakar Liongo kwa kufanya vipindi vya michezo na kuziba pengo hilo hata alipoondoka," amesema Kitenge