Yanga waisaka suluhu kupitia mkutano wao

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa tawi la Yanga la Uhuru Kariakoo, Kaisy Edwin aliliambia Mwanaspoti kwasasa amani inaweza kuvunjika kama suala la uchaguzi wao halitafikia mwafaka na kubaki kusimamiwa na TFF.

WAKATI mchakato wa uchaguzi wa Yanga ukiendelea chini ya Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imeleezwa kwamba ili amani iwepo basi ni lazima mkutano wa dhararu wa Yanga uitishwe ili kutoa maamuzi ya mwisho ya uchaguzi huo.

TFF kupitia Kamati ya Uchaguzi ilitangaza kufanya uchaguzi huo Januari 13 mwakani na sasa hatua iliyofikia ni kuweka pingamizi kwa wagombea waliofanyiwa usaili.

Mwenyekiti wa tawi la Yanga la Uhuru Kariakoo, Kaisy Edwin aliliambia Mwanaspoti kwasasa amani inaweza kuvunjika kama suala la uchaguzi wao halitafikia mwafaka na kubaki kusimamiwa na TFF.

Alisema ni lazima mkutano wa dharura wa wanachama uitishwe na ushirikishwe viongozi wa pande zote Wizara ya Michezo, Baraza la Michezo nchini, TFF na Yanga ili kusikiliza matakwa na maamuzi ya wanachama wa klabu husika.

“Hakuna anayekataa uchaguzi kufanyika, kinacholiliwa na wanachama wa Yanga ni kwamba uchaguzi usimamiwe na wanachama wenyewe na sio TFF. TFF wao wabaki kuwa waangalizi tu kama Katiba zote mbili zinavyojieleza.

“Suluhu la pamoja litatokana na wanachama wenyewe, vinginevyo ni kunyima demokrasia ya wanachama ambao ndiyo wamiliki wa klabu ya Yanga na ndiyo wenye maamuzi ya mwisho tofauti na TFF wanavyofanya hivi sasa,” alisema Kaisy.

Mwenyekiti huyo alisisitiza endapo haitafikiwa muafaka basi ataungana na viongozi wao wa matawi ambao wameweka msimamo kutoshiriki uchaguzi huo na utakuwa batili.

“Wanachama ndiyo wapiga kura, basi wana haki ya kusikilizwa maamuzi yao, hivyo muafaka usipofikiwa sidhani kama kutakuwepo na wanachama watakaoshiriki uchaguzi huo, hata mimi sitakuwa mmoja wa washiriki,” alisema Kaisy.

Alisema mgogoro mkubwa ulianza baada ya wanachama kupinga kujazwa nafasi ya Yusuf Manji ambayo imeelezwa kuwa Katiba haimruhusu kurejea kwani alijiuzulu nafasi hiyo kwa maandishi na ilipotangazwa kurejea tayari muda ulikuwa umepita.