Singida FG yajipata, Kyombo atakata Kirumba

Muktasari:

  • Singida Fountain Gate imeendeleza ubabe kwa Dodoma Jiji msimu huu, ikishinda michezo yote miwili ambayo wamekutana, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 27, mwaka jana, Singida ilishinda mabao 2-1.

Mwanza. Baada ya kuwa na matokeo mabaya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa hatimaye leo wenyeji Singida Fountain Gate wamepata ushindi muhimu huku mshambuliaji wake, Habib Kyombo akitakata kwa kuifungia mabao mawili.

Singida ambayo ilikuwa haijapata ushindi kwenye Ligi Kuu Bara tangu ilipoifunga Namungo bao 1-0 Machi 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, leo timu hiyo imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu ambao umechezwa kuanzia saa 10:00 jioni uwanjani hapo.

Kyombo ambaye alikuwa hajafunga bao kwenye Ligi tangu Januari, mwaka huu amefunga mabao hayo mawili na kuipa ushindi timu yake katika dakika ya nane kwa mkwaju wa penalti baada ya kiungo mshambuliaji Enock Atta kuangushwa kwenye eneo la hatari, huku lingine akilifunga kwa kichwa katika dakika ya 83.

Kyombo sasa amefikisha mabao sita kwenye Ligi Kuu msimu huu huku kinara wa mabao wa ligi hiyo, akiwa ni Aziz Ki wa Yanga mwenye mabao 15 akifuatiwa na Feisal Salum wa Azam FC mwenye mabao 14.

Ushindi huo ambao ni wa kwanza kwa kocha Ngawina Ngawina akiiongoza timu hiyo baada ya Jamhuri Kihwelo 'Julio' kutimka, umeipandisha nafasi ikitoka ya 11 hadi ya nane kwa kufikisha alama 29, huku ikiishusha Dodoma Jiji kutoka nafasi ya nane hadi ya 10.

Singida Fountain Gate imeendeleza ubabe kwa Dodoma Jiji msimu huu, ikishinda michezo yote miwili ambayo wamekutana, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 27, mwaka jana, Singida ilishinda mabao 2-1.

Kipa wa Singida Fountain Gate, Benedict Haule amepata ‘clean sheet’ (kutoruhusu bao) yake ya pili mfululizo tangu alipochukua nafasi ya Beno Kakolanya Aprili 14, mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Yanga na kuruhusu mabao 3-0. Clean sheet ya kwanza ikiwa ni dhidi ya Mashujaa mchezo uliomalizika kwa suluhu.

Beki wa kulia wa Singida Fountain Gate, Kelvin Kijiri amecheza mchezo wake wa kwanza baada ya kutoka kwenye majeraha tangu alipoumia Februari 28, mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Azam huku akikosa mechi saba. Leo aliingia katika dakika ya 75 akichukua nafasi ya beki, Biemes Carno ambaye alishindwa kuendelea kutokana na majeraha.

Baada ya ushindi huo, kocha Ngawina amesema matokeo hayo yanaleta morali kwenye kikosi chake kuelekea michezo mitano iliyobaki ya ligi ili kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nzuri.

Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope, amesema kukosa umakini katika safu yake ya ushambuliaji ndiyo sababu kubwa ya kupoteza mchezo wa leo, kwani wametengeneza nafasi nyingi lakini hazikutumiwa ipasavyo.