Yanga ifurahie kipigo cha Simba

Tuesday July 14 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

KABLA ya mechi na Simba, Kocha wa Yanga, Luc Eymael alitangaza kwamba mchezo huo utakuwa na matokeo ya kushangaza akimaanisha kwamba kikosi chake kingeshinda tena na kuushangaza umma, lakini mambo yakawa tofauti.

Yanga ililala kwa mabao 4-1 na kukumbana na matokeo ya kushangaza ambayo hakuna shabiki wao aliyeyatarajia kutokana na fomu ya kikosi chao katika mechi mbili zilizopita za watani.

Matokeo hayo ya nusu fainali ya Kombe la FA, yalifuta ndoto za Yanga kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao. Kwa mchezo ule kiufundi Yanga walikosea kwenye mambo yafuatayo:

SIMBA BORA, YANGA DHAIFU

Utakubaliana na ubora mdogo wa Yanga, lakini pia ubora mkubwa wa Simba, ila Wekundu wa Msimbazi walikuwa bora katika kila eneo. Lazima tujifunze kuheshimu mpira na uwekezaji walioufanya Simba kwenye kikosi. Katika mchezo huo ukiangalia wachezaji walijiamini sana na waliamua kuumiliki mchezo huo kwa ubora wa mchezaji mmojammoja awe mzawa au wa kigeni. Wote walionyesha ubora na tofauti kubwa.

Anza na safu ya ulinzi ya Simba ilitulia, ilizima kila kitu kilichokuwa kinapangwa na Yanga katika kujaribu kuathiri langoni mwao.

Advertisement

Yanga ilipiga shuti moja tu golini mwa Simba ambalo lililenga lango na ndilo lilowapa bao la kufutia machozi.

Nafasi ya kiungo ya Simba ilionekana kutulia kuliko Yanga - ubora wa watu kama Clatous Chama, Francis Kahata na viungo wawili wakabaji Jonas Mkude na Gerson Fraga walikuwa bora dhidi ya wenzao. Haikushangaza kuona viungo wao wawili wakiipatia timu hiyo mabao mawili bora ya kwanza.

Yanga haikuwa na ubora wowote mbele ya Simba. Kila kitu kwao kilionekana kizito hata ukiangalia ubora wa mchezaji mmojammoja Yanga ilionekana kuyumba zaidi.

MAJERUHI

Pengine hakukuwa na namna ya kutokana na ufinyu wa kikosi chao. Kosa ambalo Yanga walifanya ni kujilipua kwa kuwatumia wachezaji ambao hawakuwa fiti kimchezo. Anza na nahodha wao, Papy Tshishimbi. Ni mchezaji mzuri tena wa mechi kubwa kama zile lakini sio ile ya juzi. Hakuwa vyema kiafya, lakini ilishtua kuona anaanza katika mchezo huo. Yule hakuwa Tshishimbi bora aliyecheza kwa kutumia uzoefu zaidi na si ubora.

Kama haitoshi makocha wa Yanga tena wakamtumia Haruna Niyonzima ambaye hakuwa vizuri baada ya kuumia katika mechi mbili zilizopita. Hakuwa na kasi wala pasi zake hazikuonekana. Hutakosea kama utasema Yanga ilicheza pungufu muda mwingi wa mchezo, lakini pia hata uamuzi wa kumtumia beki Jafary Mohammed ambaye hakucheza mechi nyingi nalo linaungana na hilo. Hakuna jinsi unaweza kuendana na kasi ya Simba ile kwa kutumia wachezaji kama hawa, ni kubeti.

MORRISON TATIZO

Yanga walimwamini Benard Morrison, lakini walikuwa na wasiwasi naye. Mchezaji pekee aliyetarajiwa kufanya kazi kubwa ya kuisumbua Simba alikuwa yeye, ila bahati mbaya shujaa wao huyo alipoteza uhai mapema mara tu mchezo ulivyoanza. Hakuwa na makali yake ambayo yalizoweleka.

Muda mrefu alikuwa akitembea uwanjani na hata alipogusa mpira alikimbia katika msitu wa wachezaji wengi wa Simba na kuwa kama anajikaba na mbaya zaidi alipata nafasi moja bora kipindi cha pili kisha akaipoteza, alistahili kutolewa mapema. Kuna wakati baadhi ya wachezaji walionekana kumbonyeza kocha wakimaanisha amtoe kwani alikuwa anatembea tu. Kudhihirisha kwamba hakuwa siriazi na mchezo huo, alipotolewa alionyesha kutomheshimu kocha na mashabiki kwa kumsukuma mwamuzi wa akiba na kwenda zake nje ya uzio. Yanga inapaswa kusajili wachezaji wenye nidhamu kwa klabu na mashabiki.

SHIKHALO NA METACHA

Hatua ya kushangaza ni Yanga kubadili kipa ambaye alidaka vyema katika mechi au mbili zilizopita na kufanikiwa kutoruhusu bao Farouk Shikhalo, Yanga bado wanafanya makosa ya kutojua waamini kipi kwa makipa wao.

Hatua ya kumchezesha Metacha Mnata aliyeonekana kutoandaliwa kisaikolojia mapema iliwagharimu Yanga, hata ukimuuliza kipa huyo ni ngumu kwake kuamini kama alistahili kucheza mechi hiyo.

Bado inaonekana kuna kuyumba katika benchi la ufundi la timu hiyo, mwisho wa siku kazi ikiharibika kama hivyo hakuna mwingine anayestahili kulaumiwa zaidi ya Kocha Luc Eymael.

SULUHISHO

Yanga wanatakiwa kutulia kama elimu ya kusuka kikosi kipana imewafikia - tena kwa wakati muafaka ambao wanajipanga kufanya usajili mpya.

Kupitia kipigo cha mabao 4-1 walichokipata wanatakiwa kujua kwamba hawana kikosi cha kushindana kwa uwezo ambao unatarajiwa.

Akili yao mpya sasa ni kutulia na kujisuka kwa utulivu, hawatakiwi kufanya makosa kama ambayo waliyafanya huko nyuma.

Wanatakiwa kutafuta kikosi maalumu kitakachofanya kazi ya kutafuta wachezaji bora watakaokuja kurudisha ubora na heshima ya timu yao.

Advertisement