Yanga Kigelegele akesha TFF

Wednesday August 12 2020

 

By OLIPA ASSA

UKISIKIA ushabiki kindakindaki ndio huu, Anwari Mwita Wambura 'Yanga Kigelegele' anatoka Kibaha asubuhi kwa kudandia daladala kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusikiliza kesi ya winga Benard Morrison.

Kesi hiyo inayohusisha madai ya kughushi saini kwenye mkataba wake na Yanga inaendelea TFF chini ya Kamati ya Sheria, Katiba, Haki na Hadhi ya Wachezaji leo Jumatano Agosti 12, 2020 ikiwa ni siku ya tatu mfululizo.

Yanga Kigelegele amesema ameacha shughuli zake mpaka siku ambapo itapatikana hatma ya Morrison aliyesajiliwa Simba, huku akiwa na mategemeo makubwa kwamba atarejea Jangwani.

Mwanaspoti Online imekutana na Yanga Kigelegele jana Jumanne Agosti 11, 2020, saa 2:00 usiku akiwa kituo cha daladala Tabata Dampo jijini Dar es Salaam, akisubiri usafiri wa kurejea kwake Kibaha.

Alipoulizwa umetumia shilingi ngapi nauli tangu kesi ya Morrison ianze? Amejibu kuwa "Napanda bure, nadandia iwe lori, bajaji, guta ama daladala ili mladi tu nifike safari yangu, hapa kuna daladala nilipanda toka TFF, ilikuwa inaenda Tabata Kimanga, imenishusha hapa,"

Ameongeza kuwa "Najulikana, halafu nimevaa kishabiki ndio maana hata wao wakiniona wananiambia tuondoke, nimeamua kuacha kazi zangu kuhakikisha naunga mkono wanachofanya viongozi wetu kuhakikisha haki inapatikana kuhusu Morrison," amesema.

Advertisement

Kamati hiyo inaendelea na vikao vizito kuhusiana na kesi hiyo ambapo leo Jumatano walisema watatangaza hukumu baada ya jana Jumanne kuahirisha kwa kile kilichoelezwa kwamba kuna nyaraka haikukamilika kutoka Yanga.

 

Advertisement