VIDEO: Yanga, Morrison wachelewesha hukumu

NGOMA bado ngumu huko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya sakata la winga Bernard Morrison dhidi ya mabosi wake wa zamani Yanga kufikia siku ya pili bila hukumu kupatikana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba, Haki na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala amesema kuna nyaraka upande wa Yanga na Morrison hazijakamilika hivyo watasubiri kesho Jumatano Agosti 12, 2020 saa 2:30 asubuhi ziwasilishwe ili kikao kianze.

“Leo tulikuwa tunategemea tungefanya maamuzi ya mwisho kwa bahati mbaya sana kuna document (nyaraka) moja muhimu ambayo haijakamilika na tunahakikisha tutaipata kesho asubuhi saa 4 tutaanza kikao na tutatoa maamuzi” amesema Mwanjala

Mwanjala amesema sakata hilo limefikia pazuri na watu wasisikilize maneno ya mtaani wasubiri hukumu ya mwisho itakayotolewa.

Mwanjala amesema nyaraka hiyo watahakikisha itapatikana kuanzia leo Jumanne jioni na hadi sasa walipofikia ni asilimia 50 kwa 50.

Suala hilo ilibidi likamilike lilianza kusikilizwa jana Jumatatu Agosti 10, 2020 na lilitarajiwa kuitimishwa leo ila limesogezwa mbele na sasa matarajio yatakuwa kesho kujua mbivu na mbichi.

Mashabiki waliendelea kujitokeza kwa wingi nje ya lango la TFF kuhakikisha hawapitwi na kila kinachoendelea.