Yanga: Kwa hali hii tungekata moto mapema kwa Simba

Thursday October 08 2020
yanga pumzi pic

MASHABIKI wa Yanga wanajiandaa kumpokea Kocha Mkuu wao, Cedric Kaze anayeelezwa anaweza kutua muda wowote kuanzia wikiendi hii kutoka Canada, lakini unaambiwa Kocha Juma Mwambusi anayeisimamia timu kwa sasa ameamua kuwanoa upyaa kina Carlinhos wenzake ili wawe fiti zaidi.

Nyota wa kikosi hicho cha Yanga wamekuwa wakilalamikiwa kwa kucheza kichovu chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu aliyetimuliwa hivi karibuni, Zlatko Krmpotic, lakini ikabainishwa ilitokana na Mserbia huyo kuwafanyisha nyota hao mazoezi ya muda mfupi, jambo lililowasukuma baadhi ya wachezaji kuamua kufanya juhudi binafsi kwa kujifua wenyewe.

Mwambusi ni kama aliyeshtukia kitu ndani ya kikosi hicho na kuamua sasa kuipika upya timu hiyo kwa kuwanoa kina Mukoko Tonombe, Carlinhos, Tuisila Kisinda na wenzao waliopo kikosini kwa kuwapigisha tizi kwa vipindi viwili kwa siku kwa muda usiopungua saa moja na nusu kwa kila kipindi.

Ipo hivi. Kocha Mwambusi baada ya kushtukia ubora mdogo wa fiziki na stamina kwa wachezaji wao, ameamua kuanza na hilo kwa kubadilisha kila kitu kilichokuwa kikifanywa na kocha aliyeondolewa.

Hatua ya kwanza ya mabadiliko ya kocha huyo mzawa ni kuitengua ratiba ya mazoezi ya kocha Zlatko na kuamua kuwakimbiza vijana hao kwa mazoezi ya mara mbili kwa siku ili kuwafanya wawe na pumzi.

Alichofanya Mwambusi ni kuwaanzishia mazoezi vijana wake kwa kujifua kuanzia asubuhi kisha ratiba hiyo uendelea tena jioni, huku ikielezwa mazoezi hayapungui dakika 90 na wakipigishwa tizi la maana kipindi hiki mechi zimesimama kupisha michezo ya kimataifa kwa timu za taifa.

Advertisement

Hapo awali Zlatko alishuhudiwa na Mwanaspoti akiwafua wachezaji hao kwa dakika 90 ikiwa ndio muda mrefu zaidi huku kwa muda wa kima cha chini amewahi kuweka rekodi akifunga mazoezi baada ya dakika 35.

Ratiba hiyo ya Zlatko iliwashtua hata wachezaji wenyewe na hivyo kuamua kufanya mazoezi binafsi kwa siri mapema alfajiri huku wengine wakifanya gym katika kujiweka fiti zaidi na ushindani wa ligi.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Mwambusi aliwaambia mabosi wake kuwa kama wachezaji hao wangekwenda na ubora huo walionao sasa mbele ya Simba pumzi ingekata mapema na kuamua kubadilisha ratiba hiyo mara tu baada ya Zlatko kutimuliwa.

Hata hivyo, kazi hiyo ambayo Mwambusi ameianza ndani ya kikosi hicho ni kama anakuwa amemrahisishia kazi bosi wake mpya Kaze ambaye wakati wowote atatua nchini kuja kuchukua nafasi ya Zlatko.

Mwambusi alipotafutwa na Mwanaspoti ili azungumzie mabadiliko hayo ambayo inaelezwa yamepokewa kwa furaha na kina Kisinda na wenzake kwani awali waliona kama wanazinguliwa tu na Zlatko, lakini alisema hawezi kuzungumza kwani taarifa zote anazo Ofisa Habari, Hassan Bumbuli.

“Hata kama ni masuala ya kiufundi we zungumza kwanza na Bumbuli kisha atakupa ruhusa ya mimi kuongea,” alisema Mwambusi kwa kifupi.

Bumbuli alipotafutwa alisema mazoezi yanayofanywa na benchi lao la ufundi ni kuhakikisha timu inakuwa fiti zaidi kwa vile ligi bado mbichi na kwa sasa wanasubiri Kocha Mkuu wao, Kaze awasili ili kuendelea na programu zake.

Alipoulizwa ujio wa Kaze, kocha anayesifika raia wa Burundi anayeishi Canada, Bumbuli alisema kocha huyo atatua nchini muda wowote kuanzia wikiendi hii.

Advertisement