Yanga : Ligi Kuu ifutwe tu

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema pamoja na misisitizo ya TFF lakini hawatarajii kama hali itakuwa salama kwenye janga la corona ambayo mpaka jana mchana, wagonjwa walioripotiwa nchini walikuwa 20, akiwamo mmoja ambaye ni mwanachama wa Simba aliyepoteza maisha.

PAMOJA na hesabu kuibeba Simba, lakini mamlaka ya juu ya Yanga imetamka rasmi kwamba Shirikisho la Soka la Tanzania pamoja na Bodi ya Ligi wasipoteze muda wala kuhatarisha afya za mashabiki, wawape Simba Kombe lao na msimu ufutwe.

Lakini hofu kubwa imeibuka miongoni mwa vigogo wa Simba wakitafakari ni kanuni gani itatumika kuwaacha salama na ubingwa wao pamoja na timu zitakazoshuka daraja.

Janga la Corona limetishia kuendelea kwa Ligi Kuu msimu huu, huku Yanga ikishauri hata ligi ikiendelea dalili za Simba kubeba ziko wazi na hata wakitumia kigezo kwamba bingwa wa msimu uliopita ndiye awe bingwa bado bahati inaangukia kwa Simba.

Licha ya jana, Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kueleza kwamba kuna uwezekano msimu huu kwenda hadi mwishoni mwa Juni, lakini kama janga la corona litaendelea vyombo vinavyosimamia Ligi vitafanya uamuzi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo jana alisema maazimio waliyofikia awali kuhusu mwenendo wa Ligi Kuu yako pale pale, hakuna kilichobadilika.

Licha ya mkakati huo, viongozi wa klabu za Ligi Kuu wamesema kwa namna hali ilivyo, hawatarajii kama baada ya Aprili 17 Ligi itaendelea na kuishauri TFF kufuta Ligi msimu huu ambao imefika mzunguko wa 29 huku Yanga ikishauri matokeo ya msimu uliopita yanaweza pia kutumia kufanya uamuzi na maisha yakaendelea.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema pamoja na misisitizo ya TFF lakini hawatarajii kama hali itakuwa salama kwenye janga la corona ambayo mpaka jana mchana, wagonjwa walioripotiwa nchini walikuwa 20, akiwamo mmoja ambaye ni mwanachama wa Simba aliyepoteza maisha.

“TFF ingetumia msimamo wa msimu uliopita tu kuamua bingwa, aliyekuwa bingwa msimu uliopita apewe ubingwa wa msimu huu, vivyo hivyo kwa mshindi wa pili na watatu,” alisema na kuongeza.

“Hapa Ligi ilipofikia basi iahirishwe tuanze upya msimu ujao, bila shaka janga hili litakuwa limepita na timu zimejipanga vizuri, lakini kwa sasa, kusema Ligi imalizike Juni au Julai bado ni ngumu kwani hali si nzuri,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa TFF na Mtibwa.

Alisema timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja zitafutiwe utaratibu wa kushindanishwa ili kupata ambazo zitashuka, lakini hakuna garantii kwamba kufikia Juni hali itakuwa salama.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema; “Sidhani kama ni muda muafaka sasa kufanya uamuzi huo, bado muda upo. Juni bado ni mbali, tumebakiza mechi 10 za Ligi na 3 za FA, tunaweza kutafuta utaratibu mzuri zaidi kwa kushirikiana na mamlaka husika tukaona jinsi tunavyoweza kuicheza hiyo michezo kwa ufanisi na kila kitu kikawa sawa.”

Kauli ya Mwakalebela imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Lipuli, Benedict Kihwelu ambaye amesema kwa hali ilivyo kipindi hiki nchi kuwa salama na janga la corona ni majaaliwa.

“TFF ingetumia busara kuahirisha Ligi, kwani hata ikifanyika, morali ya wachezaji haitokuwepo, bado kuna taharuki kuhusu janga hili ambalo hatujui kipindi hicho TFF walichosema litakuwa liko kwenye hatua gani?

“Kilichopo ni bingwa apatikane lakini kwa kuangalia rekodi yake katika msimamo na nafasi ya wale walio nyuma yake kutwaa ubingwa ikoje, na walio kwenye hatari ya kushuka nao waangaliwe wameachana pointi ngapi?.”

Alisema kunapaswa kuwa na makubaliano ya pamoja kati ya TFF na klabu zote katika hili, Ligi ilipofikia ndiyo iwe mwisho, klabu zijipange kwa msimu ujao wakati bingwa na timu za kushuka daraja zikiwekewa utaratibu maalumu.

Aliongeza kuwa hata Kombe la Shirikisho (FA) linapaswa kufutwa na mabingwa wa msimu uliopita ndiyo waendelee kuwa mabingwa msimu huu.

Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema TFF iangalie mashirikisho mengine ya soka duniani yanafanya nini kipindi hiki, ingawa naye ameshauri Ligi ifutwe na kuanza upya.

“Matokeo ya msimu uliopita yaendelee msimu huu, ingawa hilo linahitaji uamuzi wa pamoja wa klabu,” alisema Kimbe akibainisha kwamba kuzishusha timu ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kushuka ikiwamo Mbeya City si vema wala kuipa ubingwa timu wakati mechi hazijaisha nako si sahihi.

Kocha wa Mbao, Abdul Mutiki Hajji alisema; “La hawawezi kusimamisha Ligi, basi watoe muda na Ligi ianze msimu ujao au hata mwakani, wasubiri upepo wa corona upite kabisa, sababu sasa si wachezaji tu, hata makocha tuna hofu, timu zitarudi uwanjani kinyonge kama Ligi itaendelea kipindi hiki, TFF ikubali kufanya uamuzi mgumu.”

Aliyewahi kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Mwina Kaduguda alisema ni mapema kulizungumzia hilo.

Nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema; “Afya ni kitu kingine na michezo ni kitu kingine, kwa hali ilivyo katika suala la Corona kunahitaji zaidi makubaliano ya kitaifa ili kujilinda na janga hilo.”

Alisema ni vyema suala la afya liwe mbele.