Yametimia Samatta asaini miaka minne Aston Villa

Monday January 20 2020

 

London,England. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta baada ya kusubili kwa muda hatimaye ametia saini ya kuichezea Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne.
Samatta anakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England akitokea Genk ya Ubelgiji.
Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita ilipotangazwa kuwa Samagoal atajiunga na Villa watanzania kutoka kona mbalimbali za dunia walikuwa wakisubiri kwa hamu kutimia usajili huo.
Leo saa 5 usiku klabu ya Aston Villa kupitia ukurasa wake wa twiter umemtambulisha Samatta.
Nahodha huyo wa Taifa Stars anajiunga na Villa akiwa na kibarua kizito cha kuhakikisha timu hiyo inajiondoa katika janga la kushuka daraja.
Villa kwa sasa ipo nafasi 18 katika msimamo wa ligi ya England wamemchukua Samatta kwa lengo la kumaliza tatizo lao katika safu ya ushambuliaji msimu huu.
Samagoal ameondoka Ubelgiji kwa rekodi ya kuisaidia Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kufunga mabao 25.
Pia, Samatta alithibitisha ubora wake katika Ligi ya Mabingwa akifunga mabao matatu katika hatua ya makundi na moja akifunga dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield.

Advertisement