Yaliyoibuka mkutano Bodi ya Ligi

Muktasari:

Mwanaspoti linakuletea mambo kadhaa yaliyojitokeza kwenye mkutano huo uliokwenda sambamba na uchaguzi mdogo kujaza nafasi za wajumbe.

MKUTANO wa sita uliofanywa na Bodi ya Ligi (TPLB) wiki iliyopita licha ya kwamba ulimalizika salama, lakini ulikuwa na mvutano kwa wajumbe waliokuwepo ndani ya ukumbi wa Uwanja wa Taifa ulikofanyika mkutano huo.

Mwanaspoti linakuletea mambo kadhaa yaliyojitokeza kwenye mkutano huo uliokwenda sambamba na uchaguzi mdogo kujaza nafasi za wajumbe.

WAAMUZI

Jambo hili lilikuwa ni zito katika mkutano huo baada ya baadhi ya wajumbe kufunguka kuwa waamuzi wamekuwa changamoto na wanachangia kuharibu soka nchini.

Mmoja wa wajumbe ambaye ni msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema waamuzi wamekuwa wazito kwenye utekelezaji wao wa kazi huku akisisitiza kwamba pesa imekuwa changamoto kwao.

“Mwenyekiti nimefuatilia nimegundua kwamba waamuzi wetu hawalipwi pesa, kuna tofauti ya raundi kubwa kwa waamuzi kutokulipwa pesa hizo,” alisema.

Baada ya kuzungumza hivyo, katibu mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wilfred Kidao alikubaliana na Masau huku akisema kwamba waamuzi wote wanakuwa na makubaliano maalumu kabla ya kufanya kazi.

“Kama mwamuzi anafanya makosa kisa hajapewa pesa anakosea sana taaluma yake, kwa sababu huwa tunawaambia namna ya kuwalipa na tunakubaliana,” alisema.

Aliongeza kwamba waamuzi ambao hawalipwi wakiondolewa kuchezesha mechi huwa wanalia kurejeshwa ili kuendelea kuchezesha.

Kauli hiyo iliungwa mkono na rais wa TFF, Wallace Karia aliyesema: “Mwamuzi akifanya makosa tunamuondoa kimyakimya, hakuna haja tena ya kupiga nao kelele.”

Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto alisema kuwa, “kama mwamuzi kakuambia siri ya kambi ni jambo baya, huwa tunawaambia sababu za kutolipa kwamba hatujapata pesa na hatuwalazimishi. Kwa hiyo kama wakifanya makosa wanatukosea na wanatakiwa wawe pembeni.”

Hoja hiyo ilifanya wajumbe waibue minong’ono ya chinichini ndani ya kikaochao.

SIMBA, YANGA ZAPIGWA

Klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikiutumia Uwanja wa Taifa kama uwanja wao wa nyumbani, lakini wanapokuwa katika dimba hilo huwa kuna mabango ya udhamini mwingine uwanjani.

Katika hilo, Karia alijikuta akishangaa timu hizo kukubali kucheza kwenye uwanja ambao una bango la mdhamini mwingine ambaye anafanana na wa kwao.

“Simba na Yanga wanapokea pesa kutoka SportPesa, lakini nashangaa kabisa kwa nini wanakubali kucheza sehemu kuna bango la kampuni ya kubeti nyingine, hii sio sawa kabisa,” alisema.

Karia aliongeza kwamba kwenye michuano ya CAF (shirikisho la soka Afrika), Simba walikataliwa kuvaa jezi zenye nembo ya Sportpesa, kisa kuna kampuni nyingine ya kubeti, lakini mechi hizo zinapochezwa Tanzania bango hilo la kampuni ya kubeti linafichwa.

VIWANJA VIBOVU

Mwezi uliopita baadhi ya viwanja vilifungiwa na TPLB baada ya kubainika kwamba havina ubora wa kutumika kwa ajili ya mechi za ligi, ambapo Karia aliweka msisitizo kwamba kwa timu za mikoani ambazo viwanja vyao vimewekewa zuio wanatakiwa wajipange.

“Kwa wale ambao wanatumia viwanja vya kukodi waandae mikataba kwani tutaipitia hiyo mikataba, mnatakiwa mtambue kwamba club licence (leseni ya klabu) ndio mzizi wa soka letu,” alisema.

BAJETI YAPEWA MUDA

Wakati bajeti ya bodi hiyo ikiwa inapitishwa, mjumbe na mwenyekiti wa Klabu ya Iringa United, Joel Msiba aliomba bajeti wawe wanapewa muda ili kuipitia.

“Taarifa hii tupewe wiki moja kabla ili tuipitie kwa sababu hizi ni namba na siyo kuja hapa tunakuwa kama tunaangalia,” alisema.

Wakati huohuo kiongozi wa Friends Rangers, Herry Mzozo alisema pesa ambazo zinakuwa zimebaki kwenye bajeti basi timu za Daraja la Kwanza zifikiriwe.

“Hatuna hata gari la wagonjwa (ambulance) sasa hizo pesa mtununulie sisi au tupewe viongozi, lakini Serikali waombwe hata Sh1 bilioni tugawane SDL (daraja la pili) na FDL (la kwanza) nadhani zitatusaidia kwa sababu hatuna udhamini,” alisema.

Mwenyekiti wa Pamba FC, Aleem Alibhai aliomba klabu za FDL nazo zikumbukwe katika upangaji bajeti hiyo.

“Bajeti mtufikirie na sisi, ndio maana hapa unaona kama tunasindikiza vile watu wa Ligi Kuu, rais upande wa kitaifa amefanya vizuri na ameacha alama, lakini huku FDL anatakiwa aache alama hata kama pesa hakuna basi hata kidogo,” alisema.

SDL, FDL NEEMA YANUKIA

Baada ya kukaa muda mrefu bila kuwa na wadhamini wala kuonyeshwa kwa Ligi Daraja la Kwanza na ile ya Pili, basi neema inawezakuwamulika hivi karibuni.

Mwenyekiti wa TPLB, Mnguto alisema wameanza kujipanga kuhakikisha wanawapata udhamini kwa klabu za FDL na SDL.

“Udhamini bado tunapambana lakini klabu zetu zinatakiwa zijitutumue kutafuta udhamini, nawapongeza Biashara Utd wamejitahidi wamepata udhamini wa kulipa mishahara wachezaji, ni jambo zuri,” alisema.

Kwa upande wake, Kidao alisema suala la ligi hiyo kuonyeshwa kwenye runinga limeanza kufanyiwa kazi kwa upana wake

“Mpaka Januari kuna mechi zitaonyeshwa na chaneli yetu ya TFF, lakini bado kuna baadhi ya vyombo (vya habari) tayari tumeviandikia barua ili kuonyesha ligi hizi,” alisema.