Yajayo yanafurahisha Ligi Kuu England

Muktasari:

Jurgen Klopp yeye ndiye mwenye presha kubwa. Anakabiliwa na shughuli pevu ya kuzuia uvamizi wa vigogo wa Ulaya kwenda kunasa huduma za mastaa wake Mohamed Salah na Sadio Mane

TUKUTANE mwakani. Maneno ya kujifariji unayoweza kuyasikia kutoka kwa mashabiki wa Arsenal, Man United, Man City, Chelsea na Tottenham yanapoibuka mazungumzo ya vigogo hao wa Big Six kuhusu ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Liverpool imejibebea ubingwa huo kwa pointi 99.

Man City kwenye nafasi ya pili, wamekomea na pointi 81. Man United na Chelsea kwenye nafasi ya tatu na nne, wamefunga msimu kwa kukusanya pointi 66 kila mmoja. Spurs pointi 59 na Arsenal wapo mbali zaidi kuwafikia Liverpool, wakikusanya pointi 56. Kutoka Arsenal hadi Liverpool kuna pengo la pointi 43.

Parefu. Kutoka Liverpool hadi Man City kuna pointi 18, parefu pia. Lakini, kwa Arsenal ni parefu zaidi. Kwa pointi 56 walizokusanya, Arsenal wapo karibu na timu iliyoshika mkia, Norwich City kuliko kuwafikia mabingwa Liverpool. Arsenal na Norwich zimetofautiana pointi 35.

Lakini, msimu huu umekwisha na msimu ujao unakuwa na mwanzo mpya. Kila kitu kinaanza upya. Liverpool imewaacha wenzake parefu, lakini hiyo haina maana kwamba msimu ujao watakuwa kwenye mbio za ubingwa peke yao. Bila shaka, Man City, Man United, Chelsea na pengine Spurs na hata Arsenal, makocha wao watameza mate ya akili kujua namna ya kuwadhibiti wababe hao wa Anfield.

Haina kificho makocha wa timu hizo watafungua pochi kusajili mastaa wa nguvu. Pep Guardiola atarudi kwa hasira. Ole Gunnar Solskjaer atataka kuonyesha kwamba majukumu ya kuifikisha mbali Man United yanamzidi uwezo. Frank Lampard ameshanoa panga lake kwa kuwavuta Timo Werner na Hakim Ziyech kwenye kikosi na bila ya shaka, Mourinho atapewa pesa ya kusajili sambamba na Arteta huko Emirates.

Msimu ujao utakuwa na upinzani mkali sana kwenye ligi. Kinachovutia ni kwamba hakuna staa yeyote atakayeondoka kwenye kikosi chake kwa sasa. Spurs hawatamruhusu Harry Kane aondoke. Arsenal watapambana pia kuhakikisha straika Pierre-Emerick Aubameyang anabaki Emirates.

Paul Pogba amefuta presha ya kuondoka Man United baada ya timu hiyo kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na ameshangilia jambo hilo. Hivyo, atakuwepo Old Trafford.

Shughuli ipo huko kwa Jurgen Klopp. Yeye ndiye mwenye presha kubwa. Anakabiliwa na shughuli pevu ya kuzuia uvamizi wa vigogo wa Ulaya kwenda kunasa huduma za mastaa wake. Mohamed Salah, Sadio Mane wapo kwenye hatari kubwa ya kung’olewa na miamba ya Hispania, Real Madrid na Barcelona.

Simu moja tu ya kutoka kwa miamba hiyo ya La Liga, itavuruga kabisa akili za wakali hao na hawatahitaji kuendelea kubaki Anfield, hasa ukizingatia wameshamaliza kazi ya kuweka majina yao kwenye vitabu vya rekodi kwa kuipa timu hiyo taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 30.

Hii ina maana kwamba Klopp atarudi msimu ujao akiwa kwenye presha kubwa kutetea ubingwa na kulinda mastaa wake wasiondoke. Mambo yote hayo yananogesha msimu ujao utakavyokuwa. Tukutane mwakani.