Winga atoa mbili zitakazoibakisha Mbeya City Ligi Kuu

Muktasari:

Mbeya City ipo katika hatari ya kuweza kushuka daraja ikishika nafasi ya 17 katika msimamo wa timu 20.

Winga wa Mbeya City Rehani Kibingu amesema kuna mambo mawili muhimu yanaweza kuibakisha timu yao kutoshuka daraja msimu huu.

Kibingu amesema hatua ya kikosi chao kuwa katika hatari hiyo ni kutofanya vizuri katika mechi ambazo wanaamini watavuna pointi kirahisi.

Kibingu amesema katika mechi zao tisa zilizosalia wanapaswa kutodharau timu yoyote iliyo mbele yao kama kweli wanahitaji kubaki ligi kuu msimu ujao.

"Kuna mechi tulifanya makosa sana,hakuna mechi imeniuma kama ile ya kutoa sare nyumbani tena dakika za mwisho dhidi ya Azam ambao ni kama tulishawafunga," amesema Kibingu ambaye ni winga wa zamani wa Yanga,KMC na African Lyon.

"Tulipotoka hapo tukapoteza tena na Singida United hizi ni mechi ambazo tulistahili kushinda,makosa ya namna hii hayatakiwi kufanyika katika mechi zilizosalia."

Aidha Kibingu amesema viongozi,mashabiki wa Mbeya City nao wanatakiwa kuungana na timu yao katika vita hiyo muhimu.

"Viongozi wetu na mashabiki hawatakiwi kukata tamaa tunamechi kama tano nyumbani wanatakiwa kuungana na kuwa karibu na timu yao wakati huu.

Mpaka Ligi Kuu Bara inasimama kupisha maambukizi ya Covid 19 Mbeya City inayofundishwa na kocha mzawa Amri Said inashika nafasi ya 17 katika timu 20 baada ya kushuka uwanjani mara 29 na kupoteza 13,walitoa sare 9 wakishinda 7.